Mkoa wa Morogoro ulipokea Trilioni tatu kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) fedha ambazo zilielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, wakati wa kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro kilichofanyika mkoani humo
Mhandisi Masunga amesema kuwa sekta ya Afya imetumia zaidi ya shilingi bilioni 64.6 kujenga vituo vya afya 33, zahanati 82 na hospitali za wilaya 7. Aidha fedha hizo zimetumika kununua vifaa tiba, pamoja na ongezeko la watumishi wa kada ya afya.
Sekta ya Elimu, imetumia zaidi ya shilingi bilioni 261 kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari 165, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya kati na vyuo vikuu, pamoja na utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo kwa ngazi ya msingi na sekondari.
Ameongeza kuwa, sekta ya miundombinu ya barabara za lami na changarawe pamoja na ujenzi wa madaraja, zimetumika zaidi ya shilingi bilioni 645 huku sekta ya kilimo yenyewe ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 29.6 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na viuatilifu, miradi ya skimu za umwagiliaji, pamoja na ununuzi wa vyombo vya usafiri kwa maafisa kilimo.
Aidha Mhandisi Masunga amesema sekta ya maji, imetumia zaidi ya bilioni 86.6 zikielekezwa kuazisha miradi mipya ya maji na kuboresha miradi iliyopo. Ameitaja miradi mipya iliyoazishwa kuwa ni pamoja na mradi wa bwawa la maji la Kidunda, huku sekta ya nishati ikitumia zaidi ya bilioni 737 kuboresha na kusogeza miundombinu ya umeme ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo unaimarishwa ndani ya Mkoa huo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani mbele ya wajumbe wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema, kwa kipindi cha miaka mitano, utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM imegusa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Utawala, Elimu, Afya, Kilimo, Mifugo, Uvuvi.
Aidha, amesema ilani hiyo imegusa uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, Maendeleo ya Ushirika, Maliasili na Utalii, Ardhi, Ustawi wa Jamii, Usafi na Mazingira, Masoko, Michezo na Utamaduni, pamoja na Usafirishaji, ambapo jumla ndogo ya fedha zilizotumika ni zaidi ya bilioni 618.3.
Sambamba na taarifa hiyo amesema taasisi za umma kwa kipindi cha miaka mitano, kwa upande wa sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja imepokea zaidi shilingi bilioni 948.7, sekta ya maji bilioni 422.4, na sekta ya nishati zaidi ya trilioni 1.2.
Kikao hicho kilitoka na maazimio kumi ambayo yalisomwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro Ndg. Nuru Ngereja baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kuiagiza Serikali ngazi ya Mkoa huo kuratibu mashamba yote yanayomilikiwa na watu lakini hayatumiki kwa muda mrefu, Serikali iandae mpango mkakati wa kurejesha ardhi hiyo kwa wananchi.
Mashamba hayo ni pamoja na shamba la mwekezaji wa zao la karangamiti lenye ukubwa wa zaidi ya hekta/hekari 40,000 lililoko Wilaya ya Ulanga pamoja na mashamba mengine yaliyoko Wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Mazao mbadala na ya kimkakati kama vile zao la tumbaku, michikichi, kakao, viazi mviringo, parachichi na mazao ya viuongo kama karafuu yamepewe msisitizo kulimwa Mkoani humo kulingana maeneo yaliyopo na hali ya hewa ya eneo husika.
Pia mpango madhubuti wa utoaji mikopo kqa vijana wanawake na walemavu uandaliwe ukiwa sambamba ya namna bora ya kurudisha mikopo hiyo, malipo ya posho ya vijiji na vitongoji yaliyosimama yalipwe kabla ya uchaguzi Mkuu, uboreshaji wa uwanja wa CCM Jamhuri ufanyika kwa Serikali kusgirikiana na chama