Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania TUCTA imeishauri Serikali kuangalia upya na kuweka usawa katika nyongeza ya mkupuo ya kikokotoo kwa watumishi ambao wameguswa na mabadiliko ya sheria ya watumishi wa umma kufuatia hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024-2025.
Ushauri huo umetolewa Juni 22 na Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya mkoani Morogoro katika mkutano na waandishi wa habari ambapo amesisitiza kuwa sheria hizo zitapunguza malalamiko ya wafanyakazi ambayo yamekuwepo dhidi ya kikokotoo cha awali.
“Watumishi hawa wote ni kundi moja la wafanyakazi na hii inatokana na ukweli kwamba watumishi wa umma waliokuwa PPF, mfuko wao ulikuwa imara na baada ya kuunganishwa umesaidia kufungua mfuko wa PSSSF lakini hao wanachama ndio sasa imependekezwa walipwe mkupuo wa asilimia 35 na wenzio wanalipwa asilimia 40” Amesema Nyamhokya.
Hata hivyo TUCTA imeipongeza Serikali kwa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu kutoka asilimia 33 ya sasa mpaka 40 kwa wafanyakazi waliokuwa wanalipwa asilimia 50 kabla ya mifuko kuunganishwa na asilimia 35 kwa watumishi ambao walikuwa wakipokea asilimia 25 kabla ya mifuko hiyo kuunganishwa