Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, ameipongeza na kuishukuru jamii ya kisiasa nchini kwa ushirikiano mkubwa ambao vyama vya siasa vimekuwa vikitoa kwa tume hiyo, hususan katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Akizungumza siku ya Jumamosi jijini Dodoma wakati wa kikao cha kusaini Maadili ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Jaji Mwambegele amesema kikao hicho ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu na kinadhihirisha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa huru, haki na wa amani.
“Niwapongeze kwa kukubali mwaliko wetu wa kushiriki katika kikao hiki ambacho kina umuhimu wa kipekee kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Niwashukuru viongozi wote wa vyama vya siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano tume katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali,” amesema Jaji Mwambegele.
Amebainisha kuwa moja ya majukumu hayo ni pamoja na uandaaji wa kanuni za maadili ya uchaguzi, ambazo zinatoa mwongozo wa namna vyama, wagombea na wadau wengine wanavyopaswa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria, maadili na misingi ya demokrasia.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa vyama vya siasa kutoka kote nchini pamoja na viongozi waandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lengo kuu likiwa ni kuweka misingi ya usimamizi wa kampeni na uchaguzi kwa ujumla ili kuhakikisha mazingira ya uchaguzi wa 2025 yanakuwa yenye uwazi, utulivu na mshikamano wa kitaifa.