Latest Posts

TUME YAONYA VYAMA VYA SIASA KUHUSU MAADILI YA UCHAGUZI

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amesema vyama vya siasa ambavyo vitakataa au kushindwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi vitazuiwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza Jumamosi Aprili 12, 2025 jijini Dodoma katika kikao cha kusaini maadili ya uchaguzi, Jaji Mwambegele alifafanua kuwa kifungu cha 162 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria Namba 1 ya mwaka 2024, kinabainisha wazi kuwa ni sharti la lazima kwa kila chama cha siasa na kila mgombea kusaini na kuzingatia kanuni hizo kabla ya kuwasilisha fomu za uteuzi.

“Kifungu cha 162 (2) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria namba 1 ya mwaka 2024, kinaweka sharti la ulazima kwamba kila chama cha siasa, kila mgombea, kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, serikali na tume wanapaswa kusaini na kuzingatia kanuni za maadili ya uchaguzi wakati wote wa kampeni za uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake,” alisema Jaji Mwambegele.

Aliongeza kuwa lengo la utiaji saini wa kanuni hizo ni kuhakikisha kuwa wadau wote muhimu wa uchaguzi wanathibitisha utii na uzingatiaji wa misingi ya kimaadili inayopaswa kuongoza kampeni na shughuli zote za uchaguzi.

“Tukio hili la utiaji saini si la hiari bali ni hatua muhimu ya kisheria, inayohakikisha kwamba kila chama na mgombea anakubaliana na taratibu na maadili yatakayowaongoza wakati wote wa mchakato wa uchaguzi,” alisisitiza Jaji Mwambegele.

Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ambapo vyama vyote vya siasa vilialikwa kusaini kanuni hizo mbele ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kama ishara ya dhamira ya pamoja ya kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa amani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!