Na Amani Hamisi Mjege.
Katika tamko la pamoja lililotolewa na mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Uingereza, Canada, Norway, na Uswisi, kumetolewa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka juu ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Mohamed Kibao, ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha hivi karibuni.
Tamko hilo, linaloonesha kusikitishwa na matukio ya ukatili, vifo, na kupotea kwa wanaharakati wa kisiasa nchini Tanzania, linaeleza kuwa uchunguzi wa kina ni muhimu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika na familia zao.
Mabalozi hao, wakizungumza kwa pamoja, walisema: “Tunasikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya ukatili, vifo vya kisiasa, na kupotea kwa wanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania. Tunatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na wa haki ili kuleta uwajibikaji.”
Kifo cha Kibao, ambaye alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa CHADEMA, kimezua maswali mengi katika jamii ya kisiasa nchini Tanzania. Viongozi wa chama hicho cha upinzani, Freeman Mbowe na Godbless Lema, walitoa wito wa mara moja wa kuundwa kwa tume huru ya kijaji ili kuchunguza tukio hilo.
Wanasiasa hao wamesema kuwa: “Ni muhimu uchunguzi uwe huru na wa wazi, ili ukweli upatikane na haki itendeke kwa familia ya Kibao na kwa wananchi wote wa Tanzania.”
Mabalozi wa Magharibi wameonesha uungaji mkono kwa wito huu, wakisisitiza kwamba ni muhimu kwa serikali ya Tanzania kushirikiana na wao na wadau wengine katika kufanya uchunguzi huo wa kina.
Aidha, tamko hilo limeeleza kuwa mabalozi hao wanatarajia serikali itachukua hatua madhubuti ili kufanikisha uchunguzi huo, wakimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliahidi kuhakikisha haki inatendeka.
“Tunamhimiza Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za haraka ili kufanikisha uchunguzi wa kina kwa lengo la kuhakikisha uwajibikaji kwa wahusika wa matukio haya.” Ilielezwa katika tamko hilo.
Katika mwendelezo wa tamko lao, mabalozi hao walionya kuwa kuendelea kwa matukio ya aina hii kunaweza kuathiri sana misingi ya kidemokrasia nchini Tanzania.
Pia, mabalozi hao walisisitiza umuhimu wa utulivu na ushirikiano wa kimataifa katika kipindi hiki cha changamoto. Walibainisha kuwa wataendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini, huku wakitoa msaada wa kidiplomasia kuhakikisha haki inatendeka.
Vyama vingine vya siasa nchini, pamoja na wanaharakati wa kisiasa, pia wamezungumza kuhusiana na tukio hili, wakieleza kuwa hali ya usalama kwa wanaharakati na wapinzani wa kisiasa imekuwa ikizorota.
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ambaye alishiriki katika mazishi na maziko ya marehemu Mohamed Ali Kibao, akiwa ameambatana na Makamu Mwenyekiti wa ACT bara, Isihaka Mchinjita, pamoja na ujumbe wa chama hicho, ameendelea kusisitiza wito wa kuundwa kwa Tume Huru ya Kijaji ili kuchunguza mauaji hayo na matukio mengine ya utekwaji, akieleza kuwa ni muhimu kwa haki kutendeka na ukweli kujulikana.
“Tunaendelea kusisitiza wito wetu wa kuundwa kwa Tume Huru ya Kijaji ya uchunguzi (Judicial Commission of Inquiry) kuchunguza tukio hili na mengine ya utekwaji,” aliandika kiongozi huyo kupitia mtandao wa X.
Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa yeye amemshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya uchunguzi huru na ya kiraia dhidi ya tuhuma za utekaji na mauaji ya raia nchini.
Wakili Olengurumwa amesema ni ngumu kwa wanaotuhumiwa (Vyombo vya usalama) kujifanyia uchunguzi na hivyo ni vyema Rais Samia akaongeza nguvu kwenye tume iliyoundwa (Ya Haki Jinai) kwa kuweka wajumbe wanaotoka kwenye taasisi za kiraia.
Tamko lililobeba maoni ya mabalozi wa nchi hizo za Magharibi, limetolewa kwa wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la shinikizo kutoka kwa vyama vya upinzani, mashirika ya haki za binadamu, na jamii ya kimataifa kutaka serikali ya Tanzania kuchukua hatua kali dhidi ya matukio ya hivi karibuni ya ukatili.
Kifo cha Ali Mohamed Kibao kimezua mijadala mikali kuhusu usalama wa wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu nchini Tanzania, na macho ya kimataifa sasa yanaelekezwa kwenye namna serikali itakavyoshughulikia suala hili.
Kibao inadaiwa alichukuliwa na watu wasiojulikana akiwa katika Basi la Tashrif katika maeneo ya Tegeta lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Tanga ambapo baadaye mwili wake ulikutwa ukiwa umeharibiwa vibaya maeneo ya Ununio, Dar es Salaam.