Usiku wa tarehe 27/7/2024 Jijini Arusha zimefanyika tuzo za Malkia wa Nguvu zilizoandaliwa na Clouds Media Group kwa ajili ya wanawake kwenye sekta mbalimbali kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kujenga uchumi kuinua jamii iliyowazunguka.
Katika tuzo hizo washindi ni Glory Silayo aliyeshinda tuzo ya uvumbuzi na ubunifu ambapo yeye kupitia kampuni yake anarejesha taka ngumu zinazotokana na ‘glass’ na kuzifanya bidhaa ili kutumika tena, sekta ya madini mshindi ni Lilian Rumisha ambaye yeye ni mfanyakazi wa Chuo cha Madini Arusha akiwa ni mwalimu wa kukata mawe na amefanya kazi zaidi ya miaka tisa.
Katika sekta ya mjasiriamali mshindi aliyetangazwa ni Linda Loleli, mmiliki wa karakana ya Inda Car Service, na sekta ya viwanda na biashara mshindi ni Joyce Mmari ambapo ameeleza jinsi alivyoanza na bidhaa ya viungo na sasa anamiliki kiwanda kikubwa ambacho sehemu ya bidhaa zake huuzwa nje ya nchi. Joyce alianza na mfanyakazi wa ndani mmoja lakini sasa hivi ana mtaji wa milion 450 na wafanyakazi 25.
Tuzo katika sekta ya mitindo na urembo imekwenda kwa Upendo Matimati, mfanyabiashara wa bidhaa za manukato akimiliki maduka zaidi ya Matano. Yey alianza kwa kuuza urembo, akaajiriwa na baadaye aliacha kazi ili kuanza biashara yake.
Tuzo ya sekta ya maendeleo ya biashara na chakula imekwenda kwa Vick Lavicato ambaye hivi sasa ameajiri watu zaidi ya 200 huku tuzo ya mwisho ikiwa ni ya sekta ya afya na ustawi wa jamii ambapo Getrude Kavishe ameshinda, akisema hivi sasa anamiliki shule na hospitali inayotoa huduma za kiafya.
Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha Missaile Mussa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameipongeza Clouds kwa tuzo hizo ambazo zina miaka nane tangu kuanzishwa kwake huku akieleza alipo RC makonda wakati wa salaam za mkoa wa Arusha ambapo amesema Makonda kwa sasa yupo likizo.