Latest Posts

TWCC TARIME YATOA ELIMU YA BIASHARA, MIKOPO NA MASOKO MTANDAONI

‎Na Helena Magabe -Tarime

Mkutano wa kila mwezi wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) kwa wanawake na vijana wilayani Tarime umefanyika kwa mafanikio makubwa, ukiwa umetoa elimu ya kina kuhusu masuala ya biashara, masoko, mikopo na huduma za kifedha kutoka kwa taasisi mbalimbali.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Blue Sky Hotel na kuhudhuriwa na wanachama wa TWCC kutoka ngazi ya Mkoa na Wilaya, wajasiriamali wanawake na vijana, pamoja na wafanyabiashara wachache wa kiume, ambapo CRDB Benki ilikuwa miongoni mwa wadau waliotoa mada zilizovutia washiriki wengi.

 

CRDB Yatoa Elimu ya Akaunti na Mikopo Maalum

Afisa Mahusiano wa CRDB Tarime Mjini, Bw. Sebastian Mafulu, alitoa mada katika awamu mbili ambapo alieleza aina za akaunti na dhamana za mikopo zinazopatikana benki hiyo. Katika awamu ya pili, alifafanua kuhusu mikopo maalum kwa wanawake na vijana, ikiwemo:

Mkopo wa MALKIA: Unamlenga mwanamke yeyote mwenye umri kuanzia miaka 18, ukiwa na riba nafuu ya asilimia 14, unaohitaji biashara kuwa na leseni na utambulisho halali.

Mkopo wa IMBEJU: Unalenga wanawake na vijana, hauna riba kabisa, na ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kiuchumi.

 

Masoko ya Mtandaoni Kupitia iSOKO

Praxeda Mgyabuso, Katibu Msaidizi wa TWCC Mkoa wa Mwanza na mwakilishi wa iSOKO Kanda ya Ziwa, alielezea kuhusu jukwaa la mtandaoni la iSOKO, ambalo huwezesha wanawake kutangaza na kuuza bidhaa zao bure. Alisisitiza umuhimu wa kupiga picha bora za bidhaa, kutaja maeneo zinapopatikana, na kufungua app ya iSOKO kwenye simu janja ili kuongeza mwonekano wa biashara.

“Zaidi ya wanachama 100 kutoka Mara tayari wapo iSOKO. Tarime imeanza vyema. Biashara mtandaoni si mustakabali tena, ni sasa,” alisema Mgyabuso.

TRA Yatoa Uelewa wa Kusafirisha Bidhaa Bila Kikwazo

Juliet Nyaongo (Mama Asali), mjasiriamali anayejishughulisha na asali na tiba asili, alisema elimu aliyoipata kuhusu namna ya kushughulikia changamoto kutoka TRA na kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kufuata taratibu, itamsaidia kupanua biashara yake kwa uhalali na ufanisi.

Zawadi za Shukrani Kwa Washiriki na Wadau

Katibu wa TWCC Mkoa wa Mara, Annastazia Maximillian Kirati, aliwashukuru washiriki na wadau wote waliofanikisha mkutano huo, akiwamo Matiko Foundation iliyopewa zawadi maalum kupitia Peter Magwi, Katibu wa Mbunge Easther Matiko. Wadau wengine waliotunukiwa vikombe vya shukrani ni pamoja na TRA, CRDB, Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Tarime Mji, na wengineo.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya Tarime Meja Edward Gowele, alipokea tuzo kupitia kwa mwakilishi wake Mwl. Saul Mwaisenye (Katibu Tawala).

Tahadhari Dhidi ya Njia za Panya

Saphia Chacha, Mwenyekiti wa TWCC Wilaya ya Tarime na Jukwaa la Sirari, aliwaonya wanawake dhidi ya kutumia njia zisizo rasmi (chocho) kukwepa TRA, akieleza kuwa njia hizo huwasababishia madhara kama kupoteza mizigo, kubakwa na kulipa gharama kubwa zaidi.

“Ni bora kufuata utaratibu. Kama unahitaji kusafirisha bidhaa zako hadi Kenya, Uganda au kwingineko, njoo tusaidiane kupata vibali na kusafiri kwa amani,” alihimiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!