Latest Posts

‘TWITTER REPUBLIC’ KWACHAFUKA, VIJANA WA CCM NA UPINZANI WATIFUANA KUFUNGIWA X (TWITTER)

Na Amani Hamisi Mjege.

Vuguvugu na sauti za chinichini zilianza kusikika siku chache zilizopita katika mitandao ya kijamii ikielezwa kuwa kuna kila dalili ya kufungiwa mtandao wa kijamii wa X zamani ukiitwa Twitter, kisa na mkasa ni mtandao huo kuhusishwa na kuhamasisha kile kinachotajwa kama utamaduni usiyo wa Kitanzania.

Mitandao na majukwaa mbalimbali ya kijamii ikachafuka pale Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa ulipotoa taarifa siku ya Jumanne Juni 11, 2024 ya kuitaka serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuufungia mtandao wa ‘X’ kisa jambo hilo ambalo mwenyekiti wake Mohamed Kawaida alilitaja kuharibu maadili ya vijana wa Tanzania.

Alisema jambo hilo limepokelewa kwa hisia hasi na UVCCM hivyo kuitaka serikali kuchukua maamuzi kama iliyowahi kuchukua siku za nyuma ambapo serikali ilifungia mitandao iliyokuwa ikipandisha maudhui ‘yasiyo ya Tanzania’.

Muda mchache baadaye Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu Kivuli, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa chama cha ACT Wazalendo Mhandisi Petro Ndolezi akapinga maoni ya wale wanaotaka mtandao huo ufungiwe kwa kudai kuwa mtandao huo na mitandao mingine ya kijamii kwa ujumla wake imekuwa msaada kwa vijana nchini kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitumia fursa ya uwepo wa mitandao hiyo kujitengenezea kipato hususani wakati huu ambao vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ajira.

Naam, watumiaji wa Jukwaa hilo nao hawakuwa nyuma, Siku ya Jumatano Juni 12, 2024 Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa ACT Wazalendo Rahma Mwita ambaye pia ni mtumiaji mkubwa wa mtandao huo amesema kauli za kuhimiza kufungiwa X ni njama za Serikali katika mwendelezo wa kuzuia haki ya kupata taarifa na uhuru wa kutoa maoni kupitia majukwaa mbalimbali ya habari.

“Hoja za maadili zinazotolewa na wapambe ni dhaifu, makosa ya maadili yamewekewa sheria na utaratibu wa kushughulikiwa, kama kuna Wananchi wanafanya makosa yoyote ya kimaadili mtandaoni (Twitter) zipo sheria sio kufunga mitandao, Serikali iache kujificha kwenye kichaka cha maadili, ACT Wazalendo inaungana na Watanzania waliojitokeza kupinga chokochoko za Wapambe na baadhi ya Viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, tunatoa wito kwa Wadau wote kushikamana ili kulinda uhuru wa kupata habari Nchini kwa kupinga hila zozote za Serikali kukandamiza haki hiyo” Ameeleza Rahma.

Hoja za Rahma zinaungwa mkono na mtumiaji mwingine Martin Maranja, yeye amesema kuwa kauli zinazotolewa ni za kutafuta visingizio vya kufunga mtandao wa X hivyo amewataka kauli hizo kupingwa vikali.

“Tunajua, ngono, ushoga na usagaji ni visingizio tu, lakini lengo ni kutafuta uhalali wa kufunga X. Ndiyo, mnaacha TikTok, mnapambana na X kwa sababu ya maudhui ya ngono? UVCCM, kwanza, kwanini mfikirie kufunga mitandao ya kijamii? Anauliza Martin.

Naye Roland Barnabas almaarufu kama Madenge amesema kuwa kuna haja ya serikali kujikita katika kuboresha unafuu wa matumizi ya mtandao badala ya kujikita kwenye kuifungia.

“Wakati nchi nyingine zikipambana kufanya internet iwe bure/nafuu sababu imekuwa ni chanzo cha mapato/maarifa/taarifa kwa dunia ya sasa, sisi tunapambana mitandao ifungwe eti haina maadili. Mtandaoni unapata ukitakacho kama ni mzinzi utapata video zako za ngono,fikra finyu sana” Amesema Madenge.

Kwa upande wake wakili Fatma Karume ambaye ni mtumiaji wa muda mrefu wa mtandao huo amehoji kupitia jukwaa hilo juu ya ambao wanakutana na maudhui yanayozungumzwa kuwapo X kuwa ndio wanasababisha hali hiyo.

“Nina followers 1.1 m kwenye Twitter na sijawahi kuona NGONO humu ndani. Twitter inaendeshwa na algorithms. Ukitafuta ngono utaipata tu. Swali: Unaingia Twitter kutafuta ngono tatizo Twitter au anayetafuta hiyo ngono?” Amehoji Karume.

Mwanahabari na mchechemuzi wa matumizi salama ya mitandao Imani Henrick Luvanga ameshauri njia nzuri ya kutumia mitandao mfano wa X na mingine, ambayo ni elimu ya matumizi sahihi ya kuweza kuchuja kile mtu anachotaka kukiona na kile ambacho hataki kukiona.

“Wote tunatumia hii mitandao.. kama hutaki kuviona hivyo vitu.. Safe browsing Settings zipo. Filter ya maneno na content usizotaka kuziona zipo. Ni ishu ya kuelimishana na sio kufungia hii mitandao. Labda mniambie kuna AGENDA nyingine” Ameandika Luvanga kupitia ukurasa wake wa X.

Hata hivyo bado hakuna tamko lolote kutoka serikalini juu ya mjadala huo unaoendelea kurindima katika ndimi za wapenzi na wanaokerekwa na mtandao huo wa Kijamii ambao mmiliki wake Elon Musk ameufanya kuwa jukwaa huru la kujadili mambo mbalimbali pasina kuchujwa akimuweka mwananchi kama mtoa taarifa wa kwanza sahihi na anayeaminika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!