Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesikitishwa na watu wanaofanya ubadhirifu wa fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) maeneo mbalimbali hapa nchini
Ado ametoa kauli hiyo Agosti 07.2024 wakati akiwahutubia wakazi wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera katika maeneo ya kata ya Rwamishenye ambapo amesema kuwa ipo changamoto kubwa ya ubadhirifu wa fedha hizo za wanufaika wa mpango huo ambao unawelenga wananchi maskini
Ameeleza kwamba tatizo hilo amelikuta maeneo mengi kwenye mikoa aliyopita katika ziara yake hivyo ameshangazwa kuona na Bukoba pia linajitokeza baada kupokea taarifa ya viongozi wa ACT Wazalendo ngazi ya mkoa na jimbo
“Kuna ubabaishaji mkubwa sana kwenye miradi ya TASAF na sisi tumemwambia Rais Samia nikiwa Mwanza na narudia tena kama hatoingilia kati na kuchunguza kwa umakini mkubwa mpango wa serikali wa kuzikwamua kaya maskini unakwenda nje ya mstari, kila tunakopita tumekuta ubabaishaji mkubwa sana matatizo yake makubwa ni matatu kwanza waratibu wa TASAF wanafanya ubadhirifu na upendeleo mkubwa, wanaweka majina ya watu wasiostahili, maeneo mengine tumekuta wanaweka mpaka majina ya marehemu lakini wanaostahili hawapati fedha wasiostahili ndo wanapata wakati mwingine kwa kufuata ukada ndio wanapewa fedha hizo” -Addo
Aidha, ameitaja changamoto nyingine kuhusiana na TASAF ni pamoja na utaratibu wa kuanzisha miradi ikiwemo ya ujenzi wa Barabara kutokana na mpango huo jambo alilolidai kuwa halifai kuendelea kufanyika
Katibu Mkuu huyo pia amezungumzia changamoto ya ukosefu wa kituo cha uhakika cha mabasi kwa muda mrefu mjini Bukoba akisema kwamba licha ya ahadi za muda mrefu kutoka kwa viongozi mbalimbali wa serikali na CCM bado hali imeendelea kuwa ileile ya kukosekana kwa kituo hicho, hiyo ikiwa ni sambamba na changamoto ya matibabu bure kwa watoto wa umri wa mwezi 0 hadi miaka mitano pamoja na akina mama wajawazito
Hata hivyo suala la hali ya umaskini kwa mkoa wa Kagera hakusita kulielezea kwa kuwa kiwango cha pato kiko chini ukilinganisha na takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na Benki Kuu ya Tanzania
Amedai kuwa Kagera ni mkoa uliokaliwa lasirimali za kutosha hivyo haupaswi kuendelea kuwa kwenye orodha ya mikoa inayoshika nafasi ya mwisho kwa umakini, amewahakikishia wananchi kuwa chama hicho kimejipanga vilivyo kusimama imara katika kuyashughulikia yale yote yanayoenda kinyume kwa wananchi
Katika hatua nyingine amekemea vikali kitendo cha kuwatumia makada wa chama cha mapinduzi (CCM) kuhusika na zoezi la kuandikisha daftari la wapiga kura linaloendelea akiweka wazi kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria jambo ambalo halivumiliki
Katibu Mkuu huyo ambaye katika mikutano yake anafanya zoezi la kuwasajili wanachama anaendelea na ziara yake ya siku nne mkoani Kagera
Nao viongozi wa chama ngazi ya jimbo na mkoa akiwemo Mwenyekiti wa mkoa wa Kagera Evodiu Justinian amezitaja kero kadhaa ikiwemo ya changamoto zinazojitokeza kwenye vituo vya kuandisha daftari la wapiga kura hasa ugomvi wa makada wa vyama vya siasa CCM na CHADEMA wakiwabagua baadhi ya watu kutokuandikishwa, kodi kubwa kwa wafanyabishara wadogo, wingi wa vizuizi Barabarani na zaidi ubadhirifu wa miradi ya TASAF
Viongozi hao wametoa angalizo kwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Bukoba kutokufumbia macho ‘chokochoko’ hizo kwani zinaweza kuleta uvunjivu wa amani kama hazitodhibitiwa.