Mwananchi wa Kata ya Ikobe, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Samwel Ifrahimu, ameeleza kuwa ubovu wa barabara katika kijiji chao umekuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi kuamini na kujifunza imani za kishirikina, ikiwemo madai ya kutumia usafiri wa ungo kwenda shule.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemas Maganga, kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi, Ifrahimu alisema hali mbaya ya miundombinu ya barabara imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kufika shuleni kwa wakati, na hivyo kusababisha baadhi yao kutafuta njia zisizo za kawaida, ikiwemo kuamini imani potofu.
Akijibu hoja hiyo, Mbunge Nicodemas Maganga alikiri kuwepo kwa changamoto ya miundombinu na kusisitiza kuwa Halmashauri ya Wilaya inapaswa kuchukua hatua za haraka. Alipendekeza kununuliwa kwa scavator ili kusaidia katika uchongaji na matengenezo ya dharura ya barabara hizo ili kurahisisha usafiri wa wananchi na wanafunzi.