Imeelezwa kuwa juhudi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na wadau na waandishi wa habari Zanzibar kufanya ushawishi na utetezi wa mabadiliko ya sheria zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari zimesaidia kuweka matumaini ya baadhi ya sheria hizo kufanyiwa marekebisho.
Hayo yameelezwa na wadau katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa programu ya uchechemuzi wa sheria za habari Zanzibar kilichowashirikisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Kisiwani Pemba.
Zaina Mzee ambaye ni afisa programu hiyo kutoka TAMWA ZNZ, amesema programu ya uchechemuzi wa mabadiliko ya sheria za habari zinazokwaza uhuru wa habari Zanzibar umeonesha kuleta mabadiliko ya maboresho kwenye baadhi ya vifungu vya sheria za habari ambazo ni kandamizi.
Ameeleza kuwa kupitia programu hiyo tayari TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar ZAMECO wamefanya vikao na taasisi za serikali ambazo zinahusika na utungaji wa Sheria kwa ajili ya maboresho ya vifungu vya Sheria husika.
“Kupitia mradi huu tumefanya vikao vingi na wadau wa Sheria ikiwemo tume ya kurekebisha Sheria, wajumbe wa Baraza la wawakilishi, NGOs pamoja na wandishi wa habari unguja na Pemba.” Ameeleza Zaina.
Akitoa maelezo ya tathimini ya vipindi, makaka na habari, Mohamed Khatib ambaye ni mtaalamu wa tathimini na ufuatiliaji alisema habari, makala na vipindi ambavyo vimetolewa vimeonesha ni jinsi gani waandishi wamekuwa na uwelewa wa kutosha juu vifungu vya sheria ambavyo ni kikwazo kwao.
“Tumepokea makala nyingi kutoka kwenye social media, magazeti, na vipindi vya redio. Kwa kweli zimechambua Sheria na mapungufu pamoja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kusiwe na vikwazo Kwa wandishi wa habari,” Alifafanua Mohammed.
Aidha baadhi ya waandishi wameshauri kuwa na mwendelezo wa uchechemuzi wa vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari ili sheria hizo ziweze kufanyiwa marekebisho na kuwawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao kwa uhuru.
“Waandishi wa habari tunatakiwa tutumie fursa hii ya elimu tuliyopata ya kuzijua sheria na mapungufu yake kwa kuidi kuyaandikia mapungufu yaliyopo ili yafanyiwe marekebisho.” Ameeleza mwandishi wa habari Masanja Mabula.
TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa habari ilifanya mapitio ya sheria nane (8) za habari zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari Zanzibar ikiwamo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010.