Latest Posts

UCHUNGUZI: MIILI YA DAMPO LA KWARE KENYA HAINA MAJERAHA YA RISASI ZILIZOHUSISHWA NA MAANDAMANO

Mkuu wa Uchunguzi wa Kitabibu wa Kenya Dkt. Johansen Oduora amesema kwamba hakuna maiti yoyote iliyopatikana katika eneo la kutupia taka la Kware katika vitongoji duni vya Mukuru iliyokuwa na majeraha ambayo yanaweza kuhusishwa na risasi, aidha yenye kuonekana nje au yanayotokana na uchunguzi wa miili hiyo, kama ambavyo baadhi ya wananchi wa Kenya walihusisha miili hiyo na watu waliopigwa risasi katika maandamano yanayoendelea nchini humo.

Katika taarifa aliyoitoa Dkt. Oduor siku ya Jumatano tarehe 17 Julai, 2024, miili 9 ya jinsi ya kike kati ya 13 iliyopatikana ikiwa kwenye mifuko ya gunia, imefanyiwa uchunguzi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City mnamo siku ya Jumatano kwa ushirikiano wa timu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Dkt. Oduor amesema matokeo ya uchunguzi huo yamebaini kuwa baadhi ya miili ilikosa viungo vya chini na miili mingine ikiwa na mipasuko kwenye eneo la kiuno baada ya kukatwakatwa huku moja ya miili hiyo ikiwa na majeraha makubwa kichwani na mwingine ukionekana kunyongwa.

“Baadhi ya vitu vilivyopatikana kwenye mifuko ni viungo vya chini vilivyokatwa kuanzia magoti kwenda chini na vilikuwa viwili vya kulia na viwili vya kushoto,” Amesema Dkt. Oduor.

Dk. Oduor amesema kuwa sehemu kubwa ya kazi hiyo iko katika kutambua kwa usahihi sehemu zilizokatwa, kuziunganisha na kubaini sababu ya kifo.

“Tunachukua sampuli za vinasaba (DNA) kwa lengo la kupatanisha kila kipande ili tujue tuna miili mingapi, miili ambayo imeharibika sana inakuwa vigumu sana kutaja sababu ya kifo kwa sababu kuna kile tunachokiita mabaki ya uchunguzi ambapo tishu nyingi hupotea kwa sababu ya kuharibika” Amesema Dkt. Oduor.

Kulingana na DCI, sehemu 13 za mwili za wanawake ambazo zimekatwakatwa sana na zikiwa katika hatua tofauti za kuoza zimepatikana kutoka kwenye eneo la kutupia taka la Kware kati ya Julai 11 na Julai 15, 2024.

Mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Collins Jumaisi Khalusha (33) alinaswa mnamo Julai 15 baada ya DCI kusema kwamba kufuatiliwa kwa simu ndiko kulipelekea kukamatwa kwake. DCI alidai kuwa Khalusha alikiri kuwaua wanawake 42 tangu 2022 lakini hali ya kushangaza iliibuka baada ya Khalusha kuiambia mahakama kwamba aliteswa hadi akakiri makosa yake.

 

Washukiwa wengine wawili Amos Momanyi na Moses Ogembo walikamatwa baadaye. Momanyi alipatikana akiwa na simu na laini mbili za mtandao wa Safaricom zinazomilikiwa na mmoja wa waathirwa, Roselyn Akoth Ogongo.

Ogembo anasemekana kumuuzia Momanyi simu hiyo. Mahakama siku ya Jumatano ilikubali ombi la DCI la kuwashikilia wawili hao kwa siku 28 ili kuwaruhusu kukamilisha uchunguzi kuhusu kesi hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!