Viongozi wa dini na serikali wameutaka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuhakikisha vipimo sahihi na haki kwa walaji ili kuepusha dhuluma kwenye biashara, hatua inayoweza kusababisha madhara kwa uchumi na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa wakati wa hafla ya Iftar na Dua ya ufunguzi wa jengo jipya la WMA jijini Dodoma, hafla iliyofanyika Machi 28, 2025 na kuwahusisha wadau mbalimbali, watumishi wa Wakala wa Vipimo, viongozi wa dini, na viongozi wa serikali.
Askofu Antony Mnyashimba, Askofu wa Kanisa la Baptist na Mwenyekiti wa Madhehebu ya Kikristo Dodoma, pamoja na Shekhe Ahmad Said, Msemaji wa Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, wamesisitiza kuwa vipimo visivyo sahihi vinaweza kuleta madhara kwa walaji na uchumi wa taifa.
“Wakala wa Vipimo unapaswa kutenda haki kwa kuhakikisha hakuna udanganyifu katika biashara. Kukosekana kwa uaminifu kwenye vipimo kunasababisha hasara kwa walaji na pia kunaweza kuleta laana kwa taifa,” amesema Askofu Mnyashimba.
Kwa upande wake, Shekhe Ahmad Said amesema: “Kupima kwa haki ni sehemu ya maadili ya dini zote. Tunaiomba WMA isimamie sheria kwa uadilifu na kuhakikisha hakuna dhuluma katika vipimo.”
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bi Coletha Kiwale, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi, amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Wakala wa Vipimo na kuongeza ufanisi wa huduma.
“Jengo hili ni hatua kubwa katika kuboresha utendaji wa WMA. Tunatarajia kuona usimamizi mzuri wa vipimo ili walaji wapate haki yao,” alisema Kiwale.
CPA Saleh Chondoma, Mjumbe wa Bodi ya WMA, amesisitiza kuwa kutumika kwa jengo hilo jipya kutasaidia kuimarisha udhibiti wa vipimo na kuhakikisha wateja wanapata huduma bila usumbufu.
“Tunataka kuona vipimo vyote vinazingatia sheria na kwamba walaji hawapunjwi kwa namna yoyote. Udhibiti wa vipimo ni muhimu kwa haki ya walaji na uendelevu wa biashara halali,” amesema CPA Chondoma.