Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (BAZECHA), Hashim Juma, Oktoba 1, 2024, imeibua hisia kali na mjadala mzito kuhusu udini katika siasa za Tanzania.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika tarehe hiyo kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani, Hashim alitoa matamshi yanayoelezwa kuwa na viashiria vya udini aliposema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi wanapaswa kutumia nafasi zao kama Waislamu kufanya mambo mbalimbali nchini ikiwamo kuajiri vijana wa Kizanzibari.
“Wewe ni Muislamu, Mwinyi ni Muislamu, Wazanzibari sote ni Waislamu 98%, jambo la kwanza ni kuwapatia ajira vijana wa Kizanzibari.” Alisema Mzee Hashim.
Aliongeza kuwa serikali inapaswa kuharakisha kuunganisha Zanzibar na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) kabla ya kuchaguliwa Rais Mkristo, kauli ambayo imezua mjadala mkubwa tangu ilipotolewa.
“Hapa tuko waislamu watupu, Kikwete pale, Kassim Majaliwa pale, Samia pale, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Mahmoud Thabit Kombo muislamu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni Muislamu, Rais wa Zanzibar Muislamu, hapa ndipo pa kujiunga na OIC, Msichelewe fanyeni haraka kabla hajaja Rais mwingine Mkristo”, alisikika akizungumza Hashim.
Kauli hiyo imepokelewa kwa maoni tofauti, huku ikivuta hisia kali kutoka kwa viongozi wa chama hicho na umma kwa ujumla. Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, alieleza kupitia ukurasa wake wa X kuwa kauli hiyo ni ya hatari na inahatarisha mshikamano wa kitaifa. Lema alisisitiza kuwa siasa za udini ni sumu kwa jamii na kwamba maneno hayo yanaweza kuwa sehemu ya mikakati ya siri ambayo inapaswa kupingwa waziwazi.
“Nafikiri kuna tatizo kubwa sana. Nasikitika kuwa imetolewa na Kiongozi kutoka katika Chama changu. Nashindwa kupuuza maneno haya kwa namna yoyote ile. Maneno haya yanajengwa na mikakati wa siri ambayo wengi tunanaweza kuwa tunaiona lakini tunaogopa kuchukua hatua”, Ameandika Lema.
Chama cha Chadema pia hakikuficha hisia zake juu ya kauli hiyo. Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano, John Mrema, Oktoba 2, 2024, Chadema ilisisitiza msimamo wake wa kupinga vikali kauli zenye mwelekeo wa udini. Chama kiliweka wazi kwamba hakina nafasi ya kauli zinazovuruga umoja wa kitaifa na usawa wa Watanzania wote bila kujali dini, kabila au asili yao.
“Tunajitenga na kauli zote zilizotolewa zenye viashiria vya udini kwani huo sio msimamo wa Chama na zinapaswa kupingwa na kila mtanzania bila kujali dini, kabila au mahali alipotoka”, imeeleza taarifa ya Mrema.
Aidha, Mrema amethibitisha kuwa Chadema itachukua hatua za kikatiba na kuchunguza kauli hizo kwa kina ili kuhakikisha zinatathminiwa na mamlaka husika ndani ya chama.
Wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa matamshi ya Hashim Juma huenda yakawa yanatoa changamoto kubwa kwa siasa za vyama vya upinzani nchini Tanzania, hasa kwa Chadema ambacho kinajitahidi kujenga taswira ya chama kinachojali umoja wa kitaifa. Huku Lema na viongozi wengine wa Chadema wakitoa msimamo wa wazi kupinga udini, swali linabaki ni namna gani Chadema kama taasisi itaweza kudhibiti athari za kauli kama hizi zinazoweza kuzua mgawanyiko ndani na nje ya chama.
Kauli kama ya Hashim zinaweza pia kufungua mjadala mpana kuhusu nafasi ya udini katika siasa za Tanzania, na jinsi vyama vya siasa vinavyoweza kusimamia misingi ya usawa bila kuathiri mshikamano wa kitaifa. Kimsingi, hili ni jaribio la Chadema kudumisha umoja na usawa, huku ikipambana na changamoto za kisiasa zinazotokana na kauli ‘tata’ zinazoonekana kutamkwa na baadhi ya viongozi wake.