Na Amani Hamisi Mjege.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana, amesema kuwa hakukuwa na mawasiliano ya kutosha na ya ushirikishi kati ya wafanyabiashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika uanzishaji wa tozo (kodi) kwa bidhaa za kielektroniki kama vile simu, friji, runinga, na nyinginezo, tozo inayojulikana kama ‘eco-levy’.
Mbwana ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Biashara 360 kinachorushwa na kituo cha Star TV, kinachoongozwa na mtangazaji Edwin Odemba. Amesema kuwa wafanyabiashara wa Kariakoo wamekuwa wakilalamika kutokana na mizigo yao kuzuiwa bandarini, kutokana na tozo hiyo ambayo imeelezwa kuanzishwa na TCRA.
“Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje walifahamu kwamba kuna kodi mpya ambayo haikuwepo awali kwenye utaratibu wa kikodi, lakini hata sisi viongozi hatukupata taarifa zozote, si wafanyabiashara wala viongozi wa wafanyabiashara, hatukushirikishwa,” alisema Mbwana.
Mbwana ameongeza kuwa, licha ya wafanyabiashara kufuatilia suala hilo, majibu yaliyotolewa hayakutoa ufafanuzi wa kutosha, na hali hiyo imeendelea kuwaumiza wafanyabiashara kwani mizigo yao inakaa muda mrefu bandarini, hivyo kuongezeka kwa gharama za kuhifadhi mizigo hiyo.
Amesema changamoto kubwa katika uanzishaji wa kodi hiyo ni kutosomana kwa TCRA na TRA ambayo imesababisha mkanganyiko unaojitokeza kwa sasa.
Amesema kodi hiyo kisheria ilitakiwa itolewe na mtengenezaji na siyo mfanyabiashara ambaye ni mtu aliye katikati ya mtengenezaji na mlaji, hivyo uwepo wa tozo hiyo ni adhabu kwa wafanyabiashara.
Kutokana na changamoto hiyo, Mbwana ameomba wafanyabiashara wapewe afueni ya mizigo kuondolewa bandarini ili kuepuka gharama za bandarini ili ihifadhiwe maeneo mengine kama godauni, na hapo patafutwe nafasi ya mazungumzo kati ya TCRA, TRA.
Kutokana na hali hiyo, Mbwana ameomba mamlaka zihusike na kutoa afueni kwa wafanyabiashara ili kuruhusu mizigo yao kuondolewa bandarini ili kuepuka gharama kubwa za kuhifadhi. Pia alihimiza kuwe na mazungumzo ya kina kati ya TCRA, TRA, na wafanyabiashara kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Jambo TV tumewatafuta TCRA kwa ajili ya kufafanua zaidi kuhusiana na tozo hiyo, utekelezaji wake, na namna wafanyabiashara wameelemika kwayo, ambapo imeelekezwa tumuandikie Mkurugenzi Mkuu kwa njia ya barua pepe kwa ajili ya kupata miadi yake ya kuzungumzia suala hilo kwa kina huku tukiendelea na juhudi zingine za kuweza kumfikia.
Katika jitihada za kudhibiti uingizaji wa taka za kielektroniki (e-waste) nchini, TCRA ilianzisha mpango wa kukagua vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki kabla ya kusafirishwa kuja nchini. TCRA iliteua kampuni ya Veritas Tanzania kama wakala wa ukaguzi wa vifaa vya kielektroniki kutoka nje ya nchi ili kuthibitisha kuwa vifaa vinavyoingizwa nchini si taka za kielektroniki au vilivyopitwa na wakati.
Mwezi Machi, 2023, TCRA ilieleza kuwa imekutana na waagizaji wa bidhaa na kuwafahamisha kwamba vifaa vyao vitakaguliwa kabla ya kusafirishwa kuja nchini. Ilielezwa kuwa ukaguzi huo utaanza Mei 2023 na utaambatana na malipo ya tozo ya eco levy ambayo ni kwa ajili ya kufuatilia uingizaji wa vifaa na kufanya ukaguzi wa vifaa hivyo.
Ukaguzi huu ni utekelezaji wa kanuni za mwaka 2020 za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu viwango vya vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki na usimamizi wa taka za kielektroniki, ukilenga kuzuia madhara ya taka za kielektroniki, ambazo si tu zinaathiri mazingira, bali pia ni hatari kwa afya ya binadamu.
TCRA inakadiria kuwa kwa kipindi cha miaka 26 iliyopita, taka za kielektroniki zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 10, ikihitaji hatua kali za kudhibiti kabla ya madhara zaidi kutokea. Mnamo mwaka 2019, jumla ya tani 19,000 za taka za kielektroniki ziliripotiwa nchini, ongezeko kubwa kutoka tani 2,000 mwaka 1998. Idadi hii inatarajiwa kuendelea kuongezeka kutokana na matumizi ya vifaa vya kielektroniki kama simu.