Latest Posts

UJENZI WA UWANJA WA MAONESHO KUTOKWAMISHA NANENANE 2025 NYANDA ZA JUU KUSINI

Viongozi wa Serikali na wakuu wa taasisi mbalimbali kutoka mikoa saba ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wamekutana mkoani Mbeya kwa ajili ya kikao cha kwanza cha maandalizi ya maonesho ya wakulima (Nanenane) mwaka 2025.

Kikao hicho muhimu kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Juma Homera. Lengo kuu ni kuhakikisha maandalizi ya maonesho hayo yanaenda sambamba na ujenzi wa kisasa wa uwanja wa maonesho wa John Mwakangale, licha ya changamoto zilizojitokeza awali.

Wito wa Ushirikiano wa Viongozi na Wadau

Akifungua kikao hicho, Mhe. Makongoro Nyerere ametoa wito kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wote kuungana kwa pamoja kuhakikisha maonyesho ya mwaka huu yanafanyika kwa mafanikio makubwa.

“Huu si wakati wa kurudi nyuma. Hata kama kuna ujenzi unaoendelea, tunaagizwa na wizara ya kilimo kuendelea na maandalizi. Lazima tuonyeshe mshikamano wetu,” alisema Nyerere.

Awali, Sekretarieti ya maandalizi ilipendekeza kusitisha maonyesho ya mwaka huu ili kupisha ujenzi unaoendelea katika uwanja huo mkubwa, lakini Wizara ya Kilimo ilielekeza kuwa maonyesho hayo yaendelee kama kawaida, kwa kuzingatia mipango ya muda mfupi kama vile ujenzi wa mabanda ya muda kwa washiriki.

 

Kamati Yatamka: Ujenzi Usikatishe Harakati

Said Madito, Katibu wa Sekretarieti ya maandalizi ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, aliwasilisha mapendekezo ya kamati, akieleza kuwa licha ya changamoto ya miundombinu, wanajipanga kuhakikisha kila halmashauri inashiriki kwa kujenga mabanda ya muda kwa maeneo yaliyobomolewa.

Aidha, suala la ulinzi limezingatiwa ambapo vyombo husika vitaimarisha usalama kwenye uwanja wa maonyesho baada ya kubomolewa kwa ukuta wa zamani.

 

Mchango wa Fedha Wapandishwa kwa Maendeleo Zaidi

Katika kikao hicho, wajumbe walikubaliana kwa kauli moja pendekezo la kuongeza mchango wa halmashauri kutoka shilingi milioni 2.5 hadi milioni 4, huku sekretarieti za mikoa zikitakiwa kuchangia shilingi milioni 1 kama ilivyokuwa awali.

Wajumbe wameridhia makubaliano hayo na kuahidi kwenda kuhamasisha utekelezaji wa majukumu katika ngazi za halmashauri na mikoa.

“Ni lazima tuwe na maonyesho ya mfano mwaka huu, hata kama tutatumia mabanda ya muda. Kilimo chetu kinahitaji kuonyeshwa kwa kasi na ubunifu,” alisisitiza mmoja wa wajumbe.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!