Mkoa wa Dodoma umebainisha kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia mwaka 2023, ambapo jumla ya matukio 3,012 yaliripotiwa, yakihusisha ukatili dhidi ya watoto na watu wazima.
Takwimu kutoka Mfumo wa Taarifa za Afya za Wilaya (DHIS2) zinaonesha kwamba, kati ya matukio hayo, ukatili dhidi ya watoto ulifikia 846 (wavulana 364 na wasichana 482), huku matukio kwa watu wazima yakiwa 2,166 (wanaume 478 na wanawake 1,688).
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Dodoma, Honorath Rwegasira, ametoa takwimu hizo wakati wa mdahalo wa ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Shirika la AFNET na kufadhiliwa na Women Fund Tanzania Trust, chini ya kauli mbiu “Tukomeshe Ukatili, Tujenge Jamii Salama.”
Akizungumzia takwimu za mwaka 2024 (Januari hadi Agosti), Rwegasira amesema kuwa matukio ya ukatili yaliyoshuhudiwa ni 2,352, ambapo ukatili kwa watoto ni 629 (wavulana 271 na wasichana 358), na kwa watu wazima ni matukio 1,723 (wanaume 350 na wanawake 1,373).
Rwegasira ameeleza kuwa hatua zimechukuliwa kuimarisha huduma kwa manusura wa ukatili, ambapo kituo cha utoaji huduma jumuishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kimehudumia manusura 435 (wanaume 150 na wanawake 285) tangu kuanzishwa Januari 2023. Kituo kingine cha manusura katika Kituo cha Afya cha Makole kimetoa huduma kwa manusura 391 (wanaume 106 na wanawake 285).
Amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinachangia athari nyingi, ikiwemo mimba za utotoni, ulemavu, na kuongezeka kwa maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Wadau wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kwa jamii na msaada kwa waathirika wa ukatili, pamoja na kushirikiana katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, yanayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba. Mfano wa juhudi hizi ni shirikisho la walemavu (SHIVYAWATA), ambao wamepanga kuanza kutoa elimu kwa jamii kuanzia tarehe 1 hadi 3 Desemba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani.