Latest Posts

UKOSEFU WA MAJI NA UZIO VYATAJA CHANGAMOTO KUU KWA SHULE YA JOKATE MWEGELO

Shule ya Sekondari ya Wasichana Jokate Mwegelo, iliyoko Kisarawe mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto sugu ya ukosefu wa chanzo cha uhakika cha maji.

Hii imekuwa kero inayoathiri shule hiyo, hasa baada ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kutoka 80 mwaka 2021 ilipoanzishwa hadi zaidi ya 800 mwaka 2024.

Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Mariam Mpunga, amesema kuwa licha ya jitihada kubwa za kuboresha ufaulu wa watoto wa kike na kutokomeza daraja sifuri, shule hiyo inakabiliwa na changamoto za miundombinu.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa uzio wa shule, ambao unahitajika kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wanafunzi, hasa ikizingatiwa kwamba shule hiyo ipo pembezoni mwa kijiji cha Kibuta, Kisarawe, na imezungukwa na pori. Hali hii inawaweka wanafunzi, hususan nyakati za usiku, katika hofu ya kuvamiwa na wadudu au wanyama.

Pia, Mwalimu Mpunga ametaja changamoto za ukosefu wa makazi bora kwa walimu, maabara zisizokidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi, na kutokuwepo kwa gari la shule kwa ajili ya dharura za kiafya, kutokana na umbali wa shule hiyo na mji wa Kisarawe.

Mwenyekiti wa CCM Kisarawe, Khalfani Sika, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Jokate Mwegelo, ametangaza kuwa tayari serikali imetoa Tsh. milioni 90 kwa ajili ya ukamilishaji wa bwalo la shule na Tsh. milioni 30 kwa ajili ya upanuzi wa maabara. Aidha, ametoa rai kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe kuhakikisha inatenga bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga uzio shuleni ili kuwapa wanafunzi wa kike mazingira salama ya kujifunza.

Naye Afisa Elimu wa Idara ya Sekondari, Mwalimu Editha Fue, amewasihi wazazi kuchukua jukumu la kuwalinda wanafunzi dhidi ya ukatili na vishawishi hatarishi wawapo majumbani. Amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuendeleza yale mazuri waliyoyapata shuleni.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Jokate Mwegelo (Bweni) ilianzishwa mwaka 2021 kufuatia kampeni ya Tokomeza Zero Kisarawe iliyoanzishwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa wakati huo, Jokate Mwegelo. Kampeni hiyo ililenga kuondoa kabisa daraja sifuri katika matokeo ya sekondari na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike. Tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo imeshatoa wahitimu wa kidato cha sita kwa awamu mbili (2023 na 2024) bila mwanafunzi yeyote kupata daraja sifuri. Mwaka huu wa 2024, inatarajiwa kutoa wahitimu wa kidato cha nne kwa mara ya kwanza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!