Latest Posts

UN: ZAIDI YA WATU ELFU 16 WAMEPOTEZA MAISHA HAITI

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba zaidi ya watu elfu 16 wamepoteza maisha huko Haiti tangu mwaka 2022, kutokana na ghasia za magenge ya uhalifu, huku wengine milioni 1.3 wakiyahama makazi yao hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.

‎Hayo yanajiri hivi karibuni, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupitisha azimio la kuongeza walinda usalama nchini Haiti kuungana na wale kutoka Kenya, kukabiliana na makundi hayo yenye silaha.

‎Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk, ameliambia Baraza la Haki za Kibinadamu huko Geneva kwamba, “Nusu ya watu, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 3.3, wanahitaji msaada wa kibinadamu”.

‎Amesema zaidi kwamba, juhudi za kurejesha usalama nchini humo zinahitajika ili kulinda haki za binadamu, akionya kuhusu msururu wa vurugu unaohusisha magenge, watu na vikosi vya usalama.

‎”Tangu mwezi Machi, Serikali imeongeza matumizi ya ndege zisizo na rubani katika operesheni zake za kupambana na magenge huko Port-au-Prince, Mwezi Septemba mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 559, wakiwemo watoto 11”, ameongeza Turk huku akisema mauaji hayo ni kinyume cha sheria.

‎Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2023 liliidhinisha kuundwa kwa Misheni ya Kimataifa ya Usalama (MMAS), inayoongozwa na Kenya, kusaidia polisi wa Haiti walioshindwa kukabilina na magenge hayo.

‎Kutokana na kutokuwa na vifaa vya kutosha, ufadhili wa chini, na maafisa elfu moja tu kati ya elfu 2,500 wanaotarajiwa, matokeo yake hali imekuwa mbaya kuliko ilivyotarajiwa.

‎Haiti, taifa linalotajwa kuwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi katika bara la Amerika, limekumbwa na vurugu za magenge yanayoshutumiwa kwa mauaji, ubakaji, na utekaji nyara.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!