Latest Posts

UNICEF YAIMWAGIA SIFA TANZANIA KWA UWAZI MAANDALIZI NA UTEKELEZAJI WA BAJETI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika masuala ya uwazi kwenye mchakato wa uandaaji na utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kutokana na matokeo ya utafiti uliofanywa na shirika hilo.

Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini Tanzania Elke Wisch, alipokutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano kati ya serikali na UNICEF.

Utafiti walioufanya na UNICEF utakaozinduliwa hivi karibuni unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi 16 iliyopita ambacho utafiti huo umefanyika, Tanzania imepanda viwango vya uwazi katika masuala ya bajeti kutoka asilimia 21 hadi 41 na kuzizidi nchi zote za Bara la Afrika.

Alisema kuwa katika kipindi cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi imepiga hatua kubwa katika suala la uwazi na uwajibikaji kutokana na bajeti yake kuwa na uhalisia na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara, wawekezaji, wadau wa maendeleo na taasisi za fedha.

Wisch alisema kuwa hatua hiyo inafaa kupongezwa na wadau wote wa maendeleo na kwamba matarajio ya shirika hilo ni kuona kiwango hicho kinaongezeka zaidi ili angalau kifikie zaidi ya asilimia 50, jambo ambalo alisema kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita, viwango hivyo vitafikiwa hivi karibuni.

Aidha Wisch alieleza kuwa Tanzania ina programu za chakula shuleni jambo ambalo linawasaidia wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu, lakini pia msisitizo wa lishe bora kwa watoto ni jambo muhimu ili kupambana na udumavu wa akili.

Alisema pia kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika masuala mbalimbali ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika jambo ambalo linachochea ushirikiano zaidi na mashirika ya maendeleo katika kusaidia kuchochea zaidi maendeleo ya wananchi wake katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa katika Bajeti Kuu ya mwaka wa fedha 2023/24 UNICEF iliahidi kutoa msaada wa zaidi ya dola milioni 20.3 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya uchumi wa kijamii kwenye eneo la afya, lishe, elimu, kuwalinda watoto, sera ya jamii, jinsia na mipango.

Dkt. Nchemba ameipongeza UNICEF kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zinazokuza ustawi wa jamii kupitia michango yao katika Bajeti Kuu ya Serikali zinazoelekezwa kuhudumia jamii ikiwamo afya na elimu.

Aidha Dkt. Nchemba amelishukuru shirika hilo kwa msaada wake katika masuala ya uwazi, uwajibikaji na kusaidia ushiriki wa umma katika hatua mbalimbali za maandalizi ya bajeti kupitia utafiti wao wa uwazi wa masuala ya bajeti.

Alisema kuwa tafiti hizo zimesaidia kuboresha bajeti jambo lililosaidia kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao na matumizi bora ya rasilimali na anatumaini  UNICEF itaendelea kuisaidia Serikali katika masuala ya kibajeti na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!