Latest Posts

USHIRIKIANO WA KIBIASHARA: TANZANIA YAVUTIA WAWEKEZAJI WA NIGERIA

Uwepo wa amani na utulivu, ukuaji wa kasi wa uchumi, pamoja na rasilimali nyingi zinazopatikana nchini Tanzania, vinatarajiwa kuvutia wawekezaji wengi kutoka bara la Afrika, hususan Nigeria, kuwekeza nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge, amebainisha hayo alipokutana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FIT Group kutoka Nigeria, Chief Loretta Aniagolu, kwa mazungumzo ya uwekezaji.

Katika ziara yake iliyofanyika mwezi Juni 2024 kwenye Kongamano la Uwekezaji kati ya Nigeria na Tanzania, Dkt. Mahenge alisema kuwa kongamano hilo lilitumika kama jukwaa muhimu la kuwaeleza wawekezaji wa Nigeria fursa lukuki za uwekezaji zilizopo Tanzania.

“Tulitumia Kongamano hilo kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini ili kuvutia Wanigeria wenye mitaji mikubwa. FIT Group wameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa Nyumba za Biashara (Real Estate),” alieleza Dkt. Mahenge.

Aidha, Dkt. Mahenge aliongeza kuwa ana imani kubwa na uwezo wa bara la Afrika kujitosheleza kwa mitaji ya uwekezaji. Alionesha matumaini kwamba Tanzania itaendelea kuvutia wawekezaji wengi kutoka Afrika, na si kutoka Ulaya na mabara mengine pekee.

Kwa upande wake, Chief Loretta Aniagolu alithibitisha kwamba Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji, hasa kwa nchi za Afrika Mashariki. Aliweka wazi kuwa atashawishi Menejimenti na Bodi ya Kampuni ya FIT Group kukamilisha uwekezaji wao katika sekta ya Majengo ya Biashara.

Pia aliahidi kuhamasisha kampuni nyingine za Nigeria kuja kuwekeza Tanzania, akisisitiza kwamba uwekezaji Tanzania unalindwa na kuungwa mkono kwa karibu na Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!