Latest Posts

UTEKAJI NYARA KENYA: FAMILIA ZALIA WAPENDWA WALIOPOTEA, POLISI KIKAANGONI

Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya, Inspekta Jenerali Douglas Kanja, amekanusha madai kwamba maafisa wa polisi wanahusika na vitendo vya utekaji nyara nchini. Katika taarifa yake, Kanja amesisitiza kuwa hakuna kituo cha polisi nchini kinachowashikilia watu wanaodaiwa kutekwa.

“Kwa uwazi, jukumu la Kikatiba la Jeshi la Polisi la Taifa si kuteka nyara bali kuwakamata wahalifu,” amesema Kanja

Kanja ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu mtu yeyote aliyepotea kuwasilisha ripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu. Amfafanua kuwa utaratibu uliowekwa chini ya Amri za Kudumu za Huduma unahitaji kwamba kila kukamatwa kurekodiwe katika Kitabu cha Matukio (Occurrence Book) kwa ajili ya kupelekwa mbele ya mahakama.

“Vinginevyo, watuhumiwa waachiwe kutoka kizuizini ikiwa hawakidhi vigezo vya kisheria,” ameongeza.

Inspekta Jenerali amewataka Wakenya kutumia haki yao ya kujieleza kwa uwajibikaji, akisisitiza kuwa madai haya yanakusudia kuharibu sifa ya Jeshi la Polisi la Taifa.

“Tunatoa wito kwa umma kuepuka kusambaza habari za uongo, za kutungwa, zenye nia mbaya, za kuchukiza, zisizo na msingi, na zisizothibitishwa zinazolenga kuharibu taswira na heshima ya Jeshi la Polisi la Taifa,” amesema Kanja.

Kanja alibainisha kuwa suala la utekaji linaendelea kuchunguzwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi Huru (IPOA) pamoja na taasisi nyingine huru.

Taarifa yake inakuja wakati ambapo nchi hiyo inakumbwa na msururu wa matukio ya utekaji nyara, huku familia nne zikiwa katika mateso kufuatia kutoweka kwa wapendwa wao wanaodaiwa kutekwa

Katika tukio la hivi karibuni, mchoraji vibonzo Kibet Bull, kwa jina halisi Gideon Kibet, ameripotiwa kutoweka. Familia yake pia imeeleza kuwa kaka yake, Rony Kiplangat, amepotea tangu Jumamosi.

Wengine waliotajwa kutoweka ni Bernard Kavuli, Peter Muteti, na Billy Mwangi, ambapo video za watu hawa wakichukuliwa kwa nguvu zimeonekana kwenye majukwaa ya vyombo vya habari. Vijana hawa wa Kenya walitoweka baada ya kuchapisha maoni tata kwenye mitandao ya kijamii.

Matukio haya yamezua ghadhabu kote nchini Kenya, huku polisi wakituhumiwa kuwakamata kwa nguvu watumiaji wa mitandao ya kijamii. Mnamo Jumatano, Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi Huru (IPOA) ilisema kuwa imepokea ripoti za utekaji nyara unaodaiwa kufanywa na polisi.

Kwa sasa, hatua zinazoelezwa za uwajibikaji zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha ukweli unapatikana. Wakati huo huo, umma umehimizwa kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa za kina juu ya matukio haya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!