Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imegundua tofauti kubwa ya viwango vya utekelezaji wa miradi kati ya taasisi za umma au za serikali na miradi inayotekelezwa na halmashauri za wilaya mkoani Pwani.
Kamati hiyo imeagiza kuwepo kwa uwiano sawa wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuhakikisha kuwa viwango vya utekelezaji vinafanana katika maeneo yote.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya siku moja ya ukaguzi wa miradi ya idara ya elimu wilayani Kibaha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha kuwa kuna uwiano sawa wa utekelezaji wa miradi ya taasisi za umma na ile ya halmashauri za wilaya ili kuondoa tofauti zinazojitokeza.
“Tumegundua kuna tofauti kubwa katika utekelezaji wa miradi ya taasisi za wizara na ile ya halmashauri za wilaya. Tunataka viwango sawa vya utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha kuwa ubora wa miradi yote unalingana,” amesema Sekiboko.
Akiendelea kuelezea tofauti hizo, Sekiboko amrsema kuwa kumekuwa na ukosefu wa uwiano katika gharama zinazotumika kwenye ujenzi wa miradi, akitoa mfano wa ujenzi wa darasa la elimu ya watu wazima ambao uligharimu kati ya Shilingi milioni 26 hadi milioni 28. Hata hivyo, kiasi hicho hicho cha fedha kinatumika kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa ya halmashauri, jambo ambalo linapaswa kushughulikiwa ili kuhakikisha viwango vinavyokubalika vinatumika katika utekelezaji wa miradi ya serikali.
Katika hatua nyingine, Sekiboko alitoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya ukaguzi wa vitabu vya kufundishia ili kubaini kama vinazingatia maadili ya Kitanzania na vinaendana na malengo ya taifa la Tanzania kufikia hatua za maendeleo.
Alisisitiza kuwa vitabu vya kufundishia vinavyotumika mashuleni ni lazima vikaguliwe kwa kina na kupitishwa na kamishina wa elimu kabla ya kusambazwa shuleni.
“Tunataka mahudhui ya vitabu vyote yakaguliwe na kuwekwa muhuri wa kamishina wa elimu ili kutofautisha vitabu rasmi vya kufundishia na vile ambavyo si rasmi,” alieleza Sekiboko.
Akizungumzia vitabu vinavyotolewa kama msaada kutoka nje ya nchi, Sekiboko amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinakidhi vigezo vya elimu ya Tanzania.
“Vitabu vya misaada kutoka nchi kama India, China, na Marekani lazima vikaguliwe ili kuhakikisha vinazingatia mfumo wa elimu ya Kitanzania,” aliongeza.
Katika ziara hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ambaye aliongozana na Kamati ya Bunge, aliwatakia heri wanafunzi wa darasa la saba ambao walikuwa wakiendelea na mitihani yao ya taifa. Aliwasihi wanafunzi hao kufanya mitihani kwa uadilifu na kuepuka udanganyifu.
“Nawatakia mtihani mwema na naomba mfanye kwa uadilifu bila udanganyifu wowote,” alisema Profesa Mkenda.
Ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilihusisha ukaguzi wa Shule ya Sekondari Shimbo pamoja na Kituo cha Elimu ya Watu Wazima wilayani Kibaha, ambapo kamati hiyo ilipongeza juhudi za serikali katika kuboresha elimu ya watu wazima. Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Aloyce Kamamba, alisifu juhudi hizo na kutoa ushauri kwamba walimu maalum wapewe mafunzo zaidi ili kusaidia wanafunzi hao kwa ufanisi.