Katika kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na maafisa usafirishaji (bodaboda) wamefanya mkutano maalum kuunga mkono maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 19, 2025.
Mkutano huo ulimteua Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa CCM 2025, pamoja na Balozi Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Katibu wa Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Ally Bananga, amepongeza juhudi za UVCCM na bodaboda kwa hatua yao ya kumuunga mkono Rais Samia.
“Niwapongeze sana UVCCM Wilaya ya Kinondoni chini ya Mwenyekiti wenu Ndugu Abdulrahman Kassim na maafisa usafirishaji kwa jambo hili kubwa na la kihistoria la kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza wake, Balozi Emmanuel Nchimbi, kupeperusha bendera ya CCM 2025,” amesema Bananga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Abdulrahman Kassim, amesema tukio hilo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 ya CCM, lakini pia utekelezaji wa maazimio ya baraza la vijana kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii kumuunga mkono Rais Samia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Bodaboda Wilaya ya Kinondoni, akizungumza kwa niaba ya maafisa usafirishaji, amesema wanamuunga mkono Rais Samia kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na hatua yake ya kupunguza faini kwa makosa ya barabarani kutoka TSh 30,000 hadi TSh 10,000.
“Kwa kazi kubwa aliyofanya, sisi hatuoni mbadala wa Dkt. Samia 2025. Tutamuombea kura usiku na mchana,” amesema kiongozi huyo wa bodaboda.
Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe wa baraza la UVCCM pamoja na maafisa usafirishaji wa Wilaya ya Kinondoni.