Alhamisi Julai 25.2025 kumefanyika mkutano wa wawekezaji wa ndani ya nchi ulioandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambao umefanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, tukio hilo muhimu lilikusudia kuhamasisha na kuboresha uwekezaji wa ndani nchini Tanzania kwa kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani kuwasilisha mawazo yao na kupata msaada unaohitajika
Mkurugenzi mtendaji wa TIC Gilead Teri ametoa hotuba yenye msukumo kwa wawekezaji waliohudhuria ambapo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji wa ndani kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa, ambapo katika hotuba yake amesisitiza kuwa TIC imejitolea kuunda mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na kuhakikisha kuwa wanapata taarifa sahihi na huduma bora zinazohitajika kwa ajili ya kuendesha miradi yao kwa ufanisi
“Ninawahimiza wawekezaji wote wa ndani kutumia fursa zilizopo na kuchangamkia miradi mbalimbali ambayo TIC imeandaa kwa ajili yenu” -Teri
Aidha, ameelezea mikakati ya serikali ya kuondoa vikwazo vinavyowakabili wawekezaji wa ndani na kuboresha mfumo wa kutoa leseni na vibali ili kurahisisha mchakato wa uwekezaji
Mkutano huo umejumuisha pia mijadala na mawasilisho kutoka kwa wataalam mbalimbali, walioelezea fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda, na teknolojia huku washiriki wakipata nafasi ya kujadiliana na kubadilishana mawazo, sambamba na kupata muongozo na ushauri kutoka kwa TIC na wataalam wengine
Kwa ujumla, mkutano wa Wawekezaji wa ndani umeonyesha dhamira ya TIC na serikali ya Tanzania katika kukuza na kuimarisha uwekezaji wa ndani kwa ajili ya maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi, tukio hilo ni ishara ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya uchumi.