Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) imemuhakikishia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa ziara ya Rais Mwinyi iliyolenga kukutana na kamati ya siasa za matawi, wadi na majimbo ya Mkoa wa Mjini Makamu Mwenyekiti wa UWT Ndg. Zainab Khamis Shomari (MNEC) amesema uimara na umoja wa jumuiya ni miongoni mwa sababu zinazo kihakikishia chama hicho ushindi wa kishindo.
“Uimara wa jumuiya hii kwa kiasi kikubwa unatokana na ukaribu wake na wanawake hapa nchini. Kama jumuiya tumekuwa bega kwa bega na wanawake kwenye kila jambo linalowahusu liwe la kijamii au hata kiuchumi. Matokeo ya ushirikiano huu ndio yanatupa uhakika wa imani yetu hii na hasa tukizingatia ukweli kwamba wanawake siku zote ni hodari katika kushiriki chaguzi hizi” alibainisha.
Zaidi, Makamu Zainab amemshukuru Rais Mwinyi kwa utendaji wake wa kazi pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.