Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na Shirika la ENABEL kwa ajili ya kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 600 katika vyuo vya VETA vya mikoa ya Tanga na Mwanza kupitia Mradi wa mafunzo jumuishi wa (Inclusivities).
Makubaliano hayo yanayotarajiwa kusaidia utoaji Mafunzo yatakayounga mkono sera ya Taifa ya uchumi wa bluu na nishati jadidifu, yamesainiwa leo, tarehe 28 Machi 2025, katika ofisi za Makao Makuu ya ENABEL nchini, Masaki, jijini Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya zoezi la utiaji saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkazi wa ENABEL nchini, Bw. Koenraad Goekint, amesema utiaji saini wa makubaliano hayo utawezesha kufikiwa kwa lengo la Serikali la kuwaandaa vijana kuikabili kesho yao kwa kupata umahiri wa kiujuzi.
“Sisi ENABEL tunafahamu kwambaTanzania ni miongoni mwa nchi ndogo duniani inayokuwa huku ikiwa na mageuzi makubwa katika soko lake la ajira, ukuaji katika uchumi, huku vijana wakiwa ndio mtaji mkubwa wa nguvu kazi inayohitajika kukabiliana na mageuzi hayo, hivyo VETA ina jukumu la kuwaandaa vijana hao kwa kuwapa mafunzo yatakayotolewa kupitia makubaliano haya tunayoyasaini leo” amesema.
Akiwashukuru ENABEL kwa kukubali kuunga mkono utoaji mafunzo kupitia utiaji saini huo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Antony Kasore amesema kuanzishwa kwa mradi huo kunaunga mkono juhudi za Serikali kupitia Sera ya Taifa ya uchumi wa Bluu ya Aprili, 2024 inayotaka wananchi kupata ujuzi ili kulinda mazingira na pia kutasaidia kukuza uwiano kati ya wanawake na wanaume wanaopata mafunzo katika vyuo vya VETA nchini.
“Awali tulikuwa na asilimia 22- 30 ya wanawake wanaochukua mafunzo katika vyuo vyetu kote nchini. Kutokana na kuongezeka kwa udahili kwa sasa tunahitaji miradi kama hii ili tuweze kufikia lengo la wanawake kuwa asilimia 45 ya idadi yote ya wanafunzi wanaopata mafunzo,” amesema
Mradi huo unatarajiwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wasichana na wanawake katika fani za Umeme jua, Uungaji Vyuma. Utoaji Taka katika mifumo ya maji, Mapishi, Umeme wa Majumbani na Uvuvi, ambapo vijana 300 kutoka wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza na 300 kutoka wilaya ya Tanga, mkoani Tanga wanatarajiwa kufikiwa.