Latest Posts

VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA BILIONI 2 VYAKABIDHIWA WILAYA YA RORYA

Serikali ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara leo imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2, kutoka kwa Shirika la Maji Safi Group kwa kushirikiana na Project C.U.R.E ya Marekani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk. Khalfan Haule, kwa ajili ya kusambazwa katika vituo vya afya tisa ndani ya wilaya hiyo, vikiwa na lengo la kuimarisha huduma, hususan kwa watoto wachanga na akina mama.

Huduma kwa Watoto Wachanga Zawekwa Mbele

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Maji Safi Group, Bi. Rachel Stephen, alisema kuwa baada ya tathmini ya mahitaji, ilibainika kuwa huduma za afya kwa watoto wachanga ndizo zilikuwa na changamoto kubwa zaidi, jambo lililosababisha vituo tisa kuorodheshwa kwa ajili ya kupatiwa msaada huo.

“Maji Safi Group tuliwasilisha maombi ya vifaa tiba kwa Project C.U.R.E kutoka Marekani. Baada ya tathmini, walitembelea vituo vilivyopendekezwa na sasa tunaona matokeo yake. Tunafurahia kushiriki katika kuboresha maisha ya watu wetu,” alisema Bi. Rachel.

 

Afya ni Jukumu la Kila Mtanzania

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maji Safi Group, Dk. Bwire Chilangi, alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya changamoto za afya nchini hayawezi kuachiwa Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki mpana kutoka sekta binafsi na wadau mbalimbali.

Amesema vifaa hivi vitasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma, hususan maeneo ya mipakani ambayo mara nyingi hukumbwa na changamoto nyingi za kiafya.

Serikali Yatoa Maelekezo

Akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dk. Khalfan Haule, ameishukuru Maji Safi Group na Project C.U.R.E kwa msaada huo mkubwa, huku akitoa maagizo kwa Idara ya Afya kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kufuatiliwa kikamilifu.

Makabidhiano hayo ni sehemu ya mwendelezo wa mashirikiano kati ya mashirika ya ndani na ya kimataifa katika kusaidia sekta ya afya nchini, hasa maeneo ya pembezoni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!