Na Joel Maduka, Geita.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila amefunga rasmi mafunzo ya itikadi kwa vijana wa CCM huku akisisitiza suala zima la vijana kuzingatia usalama wao wenyewe na usalama wa nchi.
Kasendamila ametoa wito huo wakati akizungumza na zaidi ya vijana 600 ambao walikuwa kwenye mafunzo ya itikadi yaliyofanyika kata ya Nyakagomba wilayani Geita.
Amesema wao kama vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kujilinda na vitendo viovu ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha yao ya sasa na baadaye.
“Natambua vijana nyie bado taifa linawahitaji na bado mna nguvu kubwa kwa Taifa letu lakini niwaombe sana zingatieni suala la usalama wenu na wa nchi, vijana wengi wamepotea sababu ni kukosa nidhamu na kujikuta wakijiingiza kwenye makundi ambayo yameendelea kugharimu maisha yao ya kila siku” Amesema Kasendamila.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Geita, Manjale Magambo amesema uwepo wa makambi ya vijana umekuwa na faida nyingi kwa vijana kutokana na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kujikwamua kiuchumi na kusaidia kukijua chama zaidi kutokana na mafunzo ya historia ambayo yanatolewa.