Zaidi ya vijana 60 wa kata ya Mabatini wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wamefanikiwa kutoka mitaani na kupewa elimu ya ujasiriamali kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali za majumbani ikiwamo sabuni hali iliyopelekea kujiajiri.
Daniel Nemes ni mmoja kati ya vijana waliokuwa wanaishi mitaani na kujihusisha na vitendo vya uhalifu, sasa amefanikiwa kujiajiri kutokana na mafunzo ya ujasiriamali aliyopewa kupitia kampuni ya EMICHEM na hiyo ni kutokana na elimu aliyopewa na polisi kata wa kata ya Mabatini Shaban Kashakala.
Kwa upande wake polisi kata wa kata ya Mabatini Shaban Kashakala amesema kupitia elimu anayoitoa kwa makundi mbalimbali ya kupambana na uhalifu alibaini kundi la vijana wa mitaani nalo linahitaji msaada na kuamua kuwaunganisha na mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ujasiriamali ili wapate mafunzo na kuweza kujiajiri.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ya ujasiriamali ya EMICHEM Emanuel Kilato amesema tangu walipoanza mwaka 2016 wameweza kuwafundisha watu zaidi ya elfu moja ikiwamo vijana waliokuwa wanaishi mitaani ambao wameshajiajiri huku wakiwasaidia na mitaji ya kuanza shughuli zao.