Kumeibuka kizaazaa siku ya Ijumaa kwa wakazi wa majimbo ya Bondo na Msambweni nchini Kenya walipoandamana katika ofisi za wabunge wao wakitaka maelezo ya upigaji kura wao Alhamisi wakati wa mjadala wa Muswada wa Fedha wa 2024 bungeni.
Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda na mwenzake wa Msambweni Feisal Bader walipiga kura kuunga mkono Muswada tata wa Fedha wa 2024.
Uamuzi huo ulionekana kuwakera wapiga kura wao huku wananchi wakijiuliza ni nani aliyemtuma anayedaiwa kuwa mwakilishi wao kupiga kura ya ‘ndiyo’.
Huko Bondo, wakazi wenye hasira waliweka alama kwenye jeneza lililoandamana na kelele za ‘Ochanda lazima aende’ na ‘Rest in Peace Ochanda’ walipokuwa wakiimba nje ya ofisi ya mbunge.
Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionesha wakazi hao waliokasirika wakitaka kuambiwa chochote na mbunge wao huku jeneza lililoandikwa #Kataa Mswada wa Fedha wa 2024 likiwekwa nje ya mlango.
Kadhalika, kikundi cha vijana huko Msamweni, kaunti ya Kwale kilimtembelea mbunge wao kutafuta majibu ni kwa nini mbunge huyo alipiga kura ya kuunga mkono muswada huo.
Video hiyo ambayo sasa inasambaa mtandaoni ilionesha vijana hao wakiandamana nje ya ofisi hiyo yenye ulinzi mkali ambapo maafisa waliokuwa na silaha walikesha huku vijana wakisubiri mbunge atoke na kuwahutubia.
Siku ya Alhamisi muswada huo wenye utata ulisomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Kitaifa baada ya wabunge 204 kupiga kura ya kuupitisha dhidi ya Wabunge 115 walioupinga. Upigaji kura ulifanyika huku kukiwa na vizuizi vikali vya polisi kuwazuia waandamanaji kufika bungeni.