Latest Posts

VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UBUNIFU KWA AJILI YA HIFADHI YA MAZINGIRA

Vijana nchini wametakiwa kutumia ubunifu wao kuandaa miradi ya kulinda na kuhifadhi mazingira kama sehemu ya kukabiliana na changamoto ya ajira na mabadiliko ya tabianchi, kupitia mradi wa majaribio unaoratibiwa na Shirika lisilo la Kiserikali la ACORD Tanzania.

Wito huo umetolewa na Meneja Mradi wa ACORD Tanzania, Ahmed Mohammed, wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Chuo Kikuu Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) jijini Mwanza, ambapo amesema vijana wana nafasi ya kipekee ya kubuni suluhisho la mazingira linaloweza kuwatoa kwenye utegemezi wa ajira rasmi.

“Vijana wengi wako mitaani bila ajira. Badala ya kukaa tu, huu ni muda wa wao kuchangamkia fursa zilizopo katika mazingira. Mradi huu utashindanisha mawazo ya ubunifu na wazo bora litafanyiwa kazi kwa msaada wa ACORD,” alisema Mohammed.

Ameeleza kuwa vijana watakaoshiriki watawekwa katika nafasi ya kuwa mabalozi wa mazingira ili kushiriki kikamilifu katika kampeni za kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Ofisa Mazingira wa Jiji la Mwanza, David Joseph, amesema bado kuna pengo kubwa la usimamizi wa taka ngumu jijini humo. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021/22, kati ya tani 357,000 za taka zinazozalishwa kila siku, ni tani 341,000 tu ndizo zinazokusanywa ipasavyo, hali inayotoa fursa kwa vijana kushiriki katika suluhisho.

“Taka ngumu zinazobaki zisizokusanywa ni zaidi ya tani 16,000 kwa siku. Hili ni eneo la fursa kubwa kwa vijana kupitia ajira na ubunifu, kwani kupitia taka hizo pekee, zaidi ya shilingi milioni 400 huzalishwa kwa mwaka,” alisema David.

Mlezi wa wanafunzi wanaojihusisha na mazingira SAUT, Ngogo Mahinyi, amesema uongozi wa chuo utaendelea kutoa mwongozo na kusaidia vijana hao kuboresha mawazo yao ya ubunifu.

Vijana walioshiriki kwenye mkutano huo wamelipongeza Shirika la ACORD kwa kuleta mradi huo, wakisema ni dira sahihi ya kuwawezesha kuanzisha miradi yenye manufaa kwao na kwa taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!