Latest Posts

VINORD AKAMATWA AKISAFIRISHA PEMBE ZA NDOVU ZENYE THAMANI YA MIL.197+

News Njombe.

Jeshi la polisi mkoa wa Njombe linawashikilia watuhumiwa watano, mmoja kati yao akikamatwa kwa kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Shilingi milioni 197. 28 huku wengine wanne wakihusishwa na tuhuma za mauaji.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Ally Kitumbu ameeleza kushikiliwa kwao wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe Februari 13, 2025.

Amesema jeshi hilo linamshikilia Vinord Ndondole (37) mkazi wa Mbarali mkoa wa Mbeya kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali ambayo ni meno manne ya tembo akiwa ameyafunga kwenye mfuko wa kiroba akisafirisha kwa pikipiki.

Amesema uchunguzi wa kesi hiyo tayari umekamilika na mtuhumiwa amefikishwa kwenye vyombo vingine vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi kulingana na kosa linalomkabili.

“Mtuhumiwa huyu alikuwa akisafirisha meno ya tembo manne akiwa ameyafunga kwenye mfuko wa salfeti akisafirisha kwa pikipiki yenye namba za usajili MC 252 CFQ aina Snor akiwa ameyafunga kama mzigo wa kawaida anaousafirisha, meno hayo yana thamani ya Shilingi milioni 197.2”, amesema Kitumbu.

Aidha amesema jeshi hilo limewakamata watuhumiwa wanne kwa kuhusika na tukio la mauaji ya mkazi wa kata ya Kijombe Ignus Chaula (40) ambapo watuhumiwa walikodiwa kwa kulipwa fedha Sh. 700,000 ili kumuua marehemu.

Amesema marehemu aliuawa kwa tuhuma za kuhusika na imani za kishirikina ambapo watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Januari 19, 2025 katika kijiji cha Ukomola huko wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.

“Watuhumiwa hao wote wanne tayari wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao yanayowakabili”, amesema Kitumbu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!