Viongozi wa vyama vya msingi (AMCO’s) wametakiwa kutotumika kisiasa na badala yake kufanya kazi kwa weledi ili kuwasaidia wakulima.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala wakati wa jukwaa la maendeleo ya ushirika mkoa wa Mtwara ambapo amewataka viongozi wote wa AMCO’s na vyama vikuu vya ushirika ikiwemo MAMCU na TANECU kuwatumikia wanachama ambao ndio wakulima kwa uaminifu, uadilifu pamoja na kuwalipa stahiki zao kwa wakati.
Pia rai hiyo imetolewa kwa wale wote ambao wamepata elimu juu ya utumiaji wa mfumo mpya wa mauzo ya mazao unaojulikana kama TMX kutoa elimu kwa wanachama na wakulima ili waweze kujua mfumo huo unavyofanya kazi ili kuepusha taharuki.
Hata hivyo viongozi hao wametakiwa kusimamia vizuri ugawaji wa pembejeo na kufanya kazi kwa uaminifu ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho huku akiagiza bodi ya korosho nchini (CBT) kutoa taarifa kwake juu ya ugawaji wa pembejeo kila siku.
“Kitu kisichoingia akilini pembejeo zipo ghalani alafu watu hawapei, watu wa vyama vikuu, viongozi mko hapa pembejeo zipo maghalani halafu wakulima hawapewi, mimi nitachukulia watu wanasababu binafsi ambazo hatutokubali, bodi ya korosho na Wakuu wa wilaya nitataka nipate taarifa kila siku jioni, nipate taarifa ya hali ya ugawaji wa pembejeo kwa wakulima wetu kila eneo” Amesema Kanali Sawala.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) Karim Chipola amesema kuwa vyama hivyo wamepanga kuongeza uzalishaji wa zao la korosho, mbaazi na ufuta kwa kuanza kuchukua hatua ya kuanzisha mashamba makubwa ya korosho na ufuta na kuboresha huduma za kiugani kwa wakulima.
Amesema ushirika kwa pamoja wamejipanga kutatua changamoto ya kukosekana kwa wanunuzi kwenye mnada ambapo watasafirisha maafisa masoko kwenda nje ya nchi ili kuangalia masoko ya mazao hayo ili kukabiliana na changamoto za kwenye minada.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Saidi Nyengedi amewataka viongozi wa ushirika na mrajisi wa vyama vya ushirika kusimamia kikamilifu suala zima la bei ya mazao ili kuleta tija kwa wakulima.
“Mnada wa ufuta kule Songwe bei iliyonunuliwa ufuta ilikuwa Tsh. 4,000/ kwa kilo, lakini mnada wetu wa kwanza ulinunuliwa si zaidi ya Tsh. 3,400/_ niwaagize Mrajisi na viongozi wa ushirika simamieni kikamilifu, wafanyabiashara wetu siku zote hawaangalii maslahi ya mzalishaji wanaangalia tija yao kwanza, na hii ni hujuma kwa sababu wanapunguza nguvu ya mkulima kuzalisha zaidi” Amesema Nyengedi.