Latest Posts

VIONGOZI WA CCM NA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI WATAJWA KATIKA HUJUMA DHIDI YA WAGOMBEA WA ACT

Chama cha ACT Wazalendo kimeonesha wasiwasi wake juu ya kile ilichokiita hujuma zinazolenga kudhoofisha nafasi ya wagombea wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rahma Mwita, Msemaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, tarehe 7 Novemba 2024, taarifa zilizokusanywa zinaashiria vitendo vya kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi dhidi ya wagombea wa chama hicho na vyama vingine vya upinzani.

ACT Wazalendo imeeleza kuwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi na watendaji wa serikali, kwa kushirikiana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekuwa wakiwashinikiza wagombea wa ACT Wazalendo kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.

“Wasimamizi wa Uchaguzi kwenye maeneo mengi nchini wameshiriki vitendo hivi kwa kupiga simu kwa wagombea wao wenyewe au kuwapatia makada wa CCM namba za wagombea zilizojazwa kwenye fomu za kugombea. Mifano ya hili ni katika Halmashauri za Tandahimba, Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini, Kilwa, Chalinze, Kigoma Mjini, Nyamagana n.k”, ameeleza Mwita katika taarifa”, imezidi kueleza taarifa hiyo.

Aidha, ACT imedai kupokea taarifa kuhusu mipango ya kuchafua fomu za wagombea wa ACT Wazalendo ili kuwanyang’anya sifa za kugombea, na hatua za baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi kupuuza maelekezo ya Waziri wa TAMISEMI ya kuvitaka vyama kuchagua ngazi ya kudhamini wagombea wao. Kutokana na hilo chama hicho kinamtaka Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa hakuna mgombea wa ACT Wazalendo atakayeenguliwa kwa hujuma zinazotajwa.

“Tunamtaka Waziri wa TAMISEMI ahakikishe Maelekezo yake ya kuvipa vyama uhuru wa kuteua ngazi ya chini ya kudhamini wagombea yanazingatiwa katika uteuzi wa wagombea”, ameeleza Mwita.

Aidha kimemtaka Waziri atoe maelekezo ya wazi kwa wasimamizi wote wa uchaguzi kwamba waache kupokea barua za wagombea kujitoa kabla ya uteuzi kufanyika na kwamba vyama vya siasa vidharau barua hizo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!