Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni kimekagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kikatiba wa kufanya tathmini kila baada ya miezi sita huku kukibainishwa kuwa katika kipindi cha miaka minne (2020-2024), Serikali kupitia Wilaya ya Kinondoni imeendelea kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa, sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Ukaguzi huo uliofanyika Septemba 5, 2024, ulilenga kupima utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya hiyo, pamoja na kutathmini changamoto zinazokwamisha maendeleo, kwa mujibu wa CCM, lengo ni kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa wananchi zinatekelezwa kwa wakati kabla ya mwaka 2025.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbula ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha nyingi za maendeleo kwa wilaya hiyo. Amewahimiza viongozi wa wilaya kuhakikisha wanufaika wa mikopo wanaendelea kufanya marejesho kwa ufanisi, huku wakipatiwa msaada wa kuongeza mitaji yao ili kuwawezesha kukuza biashara zao.
Miradi iliyotembelewa katika ukaguzi huo ni pamoja na kikundi cha kina mama wa Bunju kinachojishughulisha na utengenezaji wa masweta, kilichopata mkopo wa Shilingi milioni 38.2, ujenzi wa barabara ya Kawe Sokoni yenye thamani ya Shilingi milioni 755.9, na kikundi cha vijana cha Chamabavi kilichokopeshwa Shilingi milioni 125 kwa ajili ya shughuli za usafirishaji.
Mwenyekiti Mkumbula pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya soko la Tandale, ambalo limepata ukarabati wa Shilingi bilioni 10.47, ili wafanyabiashara wafanye kazi zao katika mazingira salama na yenye ufanisi. Aliwataka viongozi wa wilaya kufuatilia changamoto zilizopo na kuzitatua kwa wakati.