Wananchi na viongozi wa serikali wameshauriwa kutumia takwimu za matokeo ya sensa ya watu na makazi ili kupanga miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa kipaumbele panapohitajika.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa viongozi,watendaji na wadau wa wilaya ya Moshi, yaliyofanyika katika Jimbo la Vunjo baada ya Mbunge wa Jimbo hilo kuwezesha upatikanaji wa mafunzo hayo.
Babu amesema mipango ya maendeleo inapaswa kuzingatia matokeo ya Sensa na mwenendo wa kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya zake hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwamo elimu, afya, maji na barabara.
“Sisi kama mkoa wa Kilimanjaro tumeshaanza kutumia matokeo ya Sensa 2022 katika kupanga miradi ya maendeleo kwa wananchi wetu” Amesema Babu
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Kimei ameeleza kuwa matokeo ya sensa kwa viongozi, watendaji na wadau wa wilaya ya Moshi yatasaidia kuweka mipango madhubuti ya namna sahihi ya kutoa huduma.
“Jimbo la Vunjo lina watu wengi ambao wanahitaji huduma kulingana na idadi iliyopo,matokeo haya ya sensa yatasaidia kila mtu katika eneo lake kupata keki ya Taifa yaani kufikiwa na huduma zote muhimu kama maji,afya, miundombinu,elimu na mambo mengine” Ameeleza Kimei.
Kwa upande wake Mratibu wa sensa Mkoa Kilimanjaro Albert Kulwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imejipanga kuhakikisha matokeo ya Sensa 2022 yanawafikia wadau wote katika nyanja mbalimbali ili yaweze kutumika katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kuyasambaza matokeo ya Sensa kwa wadau wote ili yatumike kuwaletea wananchi maendeleo leo hii tupo hapa Vunjo ili viongozi,wadau na wananchi wajue takwimu za mkoa,Wilaya na hasa Jimbo la Vunjo na wazitumie kujiletea maendeleo” Amesema Kakulwa.
Naye kijana aliyeshiriki mafunzo hayo Yusuf Ally Mwacha kutoka kijiji cha Rau River kata ya Kahe Magharibi ameeleza kuwa elimu aliyopata kuhusu matokeo hayo itamsaidia kufanya maamuzi ya wapi pakuweka biashara pamoja na kufahamu umuhimu wa matokeo hayo kwa Serikali katika kuwapatia Maendeleo.
Akifunga mafunzo hayo Kaimu Katibu tawala Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Jackson Masaka ameshauri viongozi wa taasisi za dini pamoja na wananchi kutumia takwimu za sensa ili waweze kupata matokea tamaniwa.
“Viongozi wa dini ukitaka kufungua Kanisa au Msikiti tumia takwimu hizi zitakusaidia kufahamu ufungue wapi huduma yako,hata wananchi ambao wanafanya biashara huwezi uza nguo za watoto wadogo eneo lenye idadi kubwa ya wazee kitakacho kusaidia ni matokeo ya takwimu hizi na utalenga eneo kwa shabaha” Alishauri
Jimbo la Vunjo lina idadi ya watu 255,368 na itakumbukwa kuwa umuhimu wa takwimu zilizotokana na sensa ya mwaka 2022 itasaidia katika kufuatilia na kutathimini mipango ya maendeleo katika majimbo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule, vituo vya kutolea huduma za afya, barabara, maji na umeme.