Na Ritha J. Mushi.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) siku ya Alhamisi imetoa tahadhari kwa vituo vyote vya afya Kusini mwa Gaza kuwa viko hatarini kutokana na ongezeko la mashambulizi ya Israel, na idadi kubwa ya majeruhi.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Ujerumani cha DW Swahili, ICRC imesema wiki iliyopita takribani ya watu 850 waliwasili hospitali ndogo katika mji wa Rafah ili kupatiwa huduma huku nusu  ya hao ni  wanawake na  theluthi moja wakiwa ni watoto.
‘’Hospitali ndogo katika mji wa Rafah imepokea idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa hospitalini kutokana na majeraha yanayosababishwa na mashambulizi’’Imesema ICRC
Aidha shirika hilo limebainisha kuwa wagonjwa wengi wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na wamekuwa wakiishi katika mazingira duni yenye msongamano wa watu na yanayokabiliwa na uhaba wa chakula na maji safi, jambo ambalo linawaweka hatarini zaidi kupata magonjwa.
Katika hatua nyingine Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kwamba umwagaji damu huko Gaza ni lazima usitishwe sasa, akiongeza kuwa raia wengi katika eneo la Palestina wamepoteza maisha yao kutokana na jibu la Israel kwa ugaidi  wa Hamas.