Latest Posts

VUGUVUGU LA KATIBA MPYA LAPAMBA MOTO, RAIA WAITAKA TUME YA WARIOBA

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Vuguvugu la upatikanaji wa katiba mpya nchini Tanzania linaendelea ambapo wananchi wameitaka serikali kuendelea na tume ya Jaji Joseph Warioba ili Tanzania ipate katiba bora itakayoendana na wakati wa sasa.

Wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii Mkoani Mbeya wametoa maoni hayo kwenye kikao cha mjadala wa wazi juu ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania. Wakili wa kujitegemea kutoka kundi la wanasheria Ezekiel Mwampaka amesema ni muhimu Tanzania kupata katiba mpya kwani ucheleweshaji wake umekuwa mkubwa sana.

“Kwanza niseme TLS (Chama cha Mawakili wa Tanganyika) tumechelewa sana, na mimi niseme tu ni muumini wa Serikali tatu, baadhi ya watu wanajiuliza Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania haitakuwa na fedha basi mjue tu hayo ni mawazo mfu kwa sababu mabillioni yapo tu yanayopotea kwa mujibu wa CAG” Amesema Wakili Mwampaka.

Kwa upande wake Agatha Daud Kaleke ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa mmojawapo mkoani humo amesema malumbano hayapaswi kushuhudiwa miongoni mwa wananchi badala yake waungane kudai katiba mpya bila ubaguzi wowote ili kufikia maendeleo endelevu.

Naye Mhandisi Maneno Sanga ameshauri wasomi ikiwamo mawakili kwamba, licha ya kuzingatia maoni ya wananchi kupitia makundi mbalimbali, pia watoke na hoja ya pamoja ili kufanikiwa kuwa na katiba iliyoboreshwa kuanzia kwenye katiba ya sasa ya mwaka 1977.

Alipopata nafasi ya kuchangia katika mjadala huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi (Sugu), amesema katiba mpya ni hitaji la wananchi la muda mrefu pamoja na tume huru ya uchaguzi.

Sugu amesema wasiotaka kupatikana kwa katiba mpya ni wanufaika wa katiba ya sasa kwa kutaka kuendelea kusalia madarakani bila uwajibikaji mzuri wa viongozi kwa wananchi mambo ambayo anasema serikali ya CHADEMA haitavumilia.

Naye Mjumbe wa bodi ya Jukwaa la Katiba Tanzania Deus Kibamba ameainisha udhaifu wa katiba ya 1977 na kuonesha umuhimu wa Watanzania kuungana kudai katiba mpya kwa  kuanzia kwenye maoni ya Jaji Joseph Sinde Warioba.

“Niwaambie mmeiona hii ni rasimu ya Jaji Warioba natamani kuibusu, kwenye nchi hii Jaji Joseph Warioba amevunja rekodi ya kufanya kazi nzuri sana ya kukusanya maoni haya, wapo watu wanaosema aliwahoji wangapi, kiukweli kwenye jambo kama hili huwezi kuwafikia watu wote lakini kwa utafiti wangu mimi binafsi watu waliotoa maoni kwa njia tatu za kumfikia Jaji Warioba, kutuma maoni au kwa namna nyingine yoyote wamefikia nusu ya Watanzania wote hapa nchini (Zaidi ya watu million 30)” Ameeleza Kibamba.

Mbobezi huyo wa masuala ya sayansi ya siasa amesema ni wakati muafaka wa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu mchakato wa katiba mpya kupitia Rasimu ya Jaji Warioba kwa kuwa Katiba ni matakwa na mali ya wananchi badala ya katiba ya sasa ambayo amesema kuwa imefanyiwa marekebisho mara kadhaa lakini bado haiendani na wakati wa sasa huku ikiwa na mamlaka makubwa kwa Rais wa nchi badala ya wananchi.

Kwa upande wake Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Wakili Francis Stolla, amesema kwa mujibu wa katiba ya sasa Rais wa Tanzania anaweza kushitakiwa kwa kosa la madai pekee lakini kwa kesi ya jinai hatakiwi kushitakiwa kwa kuwa amewekewa kinga na katiba , akieleza kuwa jambo hilo ni miongoni mwa mambo yanayotakiwa kuangaliwa kwenye katiba mpya.

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kinaendelea kuendesha mijadala ya wazi ili kuwajenga, kuwasikiliza na kupokea maoni ya wananchi kuhusu namna bora kutoka kwenye mkwamo wa Katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa ili kupata Katiba mpya ambayo inatajwa kuwa hitaji la wananchi katika uendeshaji wa taifa lao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!