Latest Posts

VYAMA 9 VYA SIASA KUSHIRIKI UCHAGUZI SERIKALI ZA VIJIJI NA VITONGOJI PERAMIHO

Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya wilaya ya Songea , Bi Elizabeth Gumbo, amevitaka vyama vya Siasa kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.

Bi Gumbo ameyasema hayo kwenye mkutano na vyombo vya habari ambao umefanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Ameeleza kuwa jumla ya vyama tisa (9) vimejitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Vyama hivyo ni CCM, CHADEMA, CUF, TADEA, ACT Wazalendo, UDP, Demokrasia Makini, NCCR Mageuzi, na TLP.

Kwa mujibu wa Gumbo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea inajumuisha jumla ya vijiji 56, na wagombea 97 wamejitokeza kugombea nafasi za uongozi kutoka vyama hivyo mbalimbali.

Aidha, jumla ya vitongoji 443 vimeorodheshwa na wagombea 556 wameshajaza na kurejesha fomu kwa ajili ya kugombea nafasi katika vitongoji hivyo.

Gumbo amebainisha kuwa zoezi la uteuzi na usikilizwaji wa rufaa linaendelea mpaka tarehe 15/11/2024 ambapo kampeni zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 20 hadi 26 Novemba mwaka huu.

“Tunawaomba vyama vyote tisa kufanya kampeni za kistaarabu kwani lengo letu ni kupata viongozi bora, na hatutarajii kuwa na changamoto au migogoro baina ya vyama wakati wa kampeni,” amesema Bi Elizabeth Gumbo.

Katika hotuba yake, Bi Gumbo pia ametoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambao wamejiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ifikapo tarehe 27 Novemba 2024s, kuanzia saa mbili kamili asubuhi, ili kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.

Ameongeza kuwa Halmashauri imejipanga kuhakikisha ‘4R’ za Mheshimiwa Rais zinafanyiwa kazi kikamilifu kwa faida ya wananchi.

Kwa ujumla, Bi Elizabeth Gumbo amesisitiza umuhimu wa amani, utulivu, na ushirikiano wa vyama na wananchi wote katika kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa amani na wenye mafanikio.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!