Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema wamepanga kufanya matengenezo katika eneo maalumu la kuhudumia shehena ya mafuta kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja na watumiaji wa bandari hiyo wa ndani na nje ya nchi.
Mrisho amesema hayo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akiongea na waandishi wa habari walipotembelea eneo hilo ambapo amesisitiza kuwa eneo hilo ni muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani.
Aidha Mrisho amesema ukarabati huo utahusisha kubadilisha bomba zinazopakua mafuta kutoka kwenye meli hadi kwenye hifadhi za mafuta zilizopo Kigamboni na unataraji kufanyika kwa siku saba za wiki ijayo.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwaondoa hofu waagizaji wa mafuta nchini kuwa ukarabati utakaofanyika katika boya la kushushia mafuta ya nishati aina ya dizel baharini kupitia bomba la TAZAMA kwamba hautakuwa na athari katika ushushaji wa mafuta huku akieleza mpango wa muda mrefu wa kuongeza ufanisi katika kuhudumia shehena za mafuta.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ina mpango mkubwa wa kujenga SRT-Single Receiving Terminal (upokeaji wa mafuta katika ghala moja) ambayo ita-accomodate shughuli zote zifanyike katika eneo moja lengo likiwa ni kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi” Amesema Mrisho.
Kwa upande wake, Meneja wa gati ya kupakulia mafuta TPA Mhandisi Yona Malago amesema matengenezo katika eneo hilo yaliyoanza tarehe 06 Juni, 2024 hayakukamilika kwa wakati kutokana na wingi wa meli zilizokuwa zikisubiri kuhudumiwa na kuepuka nchi kuingia gharama lakini pia kulinda na kuongeza ufanisi wa bandari huku wakifahamu kuwa wateja walikuwa wakisubiri nishati hiyo muhimu.
“Baada ya kuhudumia meli mbili za mafuta zinazosubiri huduma hivi sasa, tutafunga eneo hili maalumu la kuhudumia shehena ya mafuta kwa ajili ya kufanya matengenezo lakini haitaathiri shughuli za kuhudumia shehena za mafuta” Amesema Malago.
Mhandisi Malago ameongeza kuwa wao kama TPA shauku yao ni kuona eneo hilo linatoa huduma kwa ufanisi mkubwa.
Mnamo tarehe 26 Februari, 2024 Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba wa ujenzi wa matenki na miundombinu ya kupokelea, kuhifadhi na usambazaji wa bidhaa ya mafuta katika bandari ya Dar es Salaam.
Mkataba huo utagharimu Shilingi bilioni 678 mpaka kukamilika kwake na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi ishirini na nne (24) huku ukitajwa kuwa na manufaa siyo tu kwa Tanzania bali kwa nchi nyingine zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam katika kupokea bidhaa za mafuta.