Latest Posts

WAALIFU ZAIDI YA 900 WAKAMATWA MBEYA

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya operesheni, misako na doria mbalimbali zenye tija na kupata mafanikio kadhaa ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari pekee jumla ya watuhumiwa 979 wamatajwa kukamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali.

 

Baadhi ya makosa ya watuhumiwa ni mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, kujeruhi, kupatikana na nyara za serikali, kuingia nchini bila kibali, kupatikana na silaha bila kuwa na kibali na kupatikana na dawa za kulevya.

 

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi Wanyama pori [TANAPA] lilifanikiwa kuwashikilia watuhumiwa wanne, Dadrahimu Aladad [74] mkazi wa Igalako, Daud Masengwa [55] mkazi wa Mahango Ruiwa, Mkombe Mathias [34] mkazi wa Mwatenga na Dotto Daimon [39] mkazi wa Mwatenga kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno ya Tembo.

 

Watuhumiwa walikutwa wakiwa na Jino moja zima na vipande viwili vya meno ya Tembo katika mfuko wa sandarusi wakiwa wameficha nyumbani kwa mtuhumiwa Dadrahimu Aladad wakitafuta mteja na kwamba watuhumiwa ni wawindaji haramu katika hifadhi za Taifa.

Kamanda Kuzaga amesema pia polisi Mbeya inawashikilia Faraja Majengo [19] mkazi wa Kijiji cha Majengo wilayani Chunya, Fidelis Mdutu [25] na Charles Laiton Mfilinge [39] wote wakazi wa Iyowanza Wilayani Mbarali kwa tuhuma za kupatikana na silaha bunduki aina ya Gobole mbili bila kuwa na kibali cha kumiliki silaha hizo.

 

Amesema watuhumiwa walikamatwa njiani na Askari waliokuwa doria katika kijiji cha Majengo na Kijiji cha Iwalanji na walipofanyiwa upekuzi walikutwa na silaha hizo pamoja na goroli 228 ambazo huzitumia kama risasi katika silaha hiyo, Fataki 14, vipande vya Nondo 16 na Unga wa Baruti makopo mawili.

 

Taarifa hiyo ya Polisi kwa umma, imeeleza kuwa mtuhumiwa mmoja alikutwa na nyara za Serikali bila kuwa na kibali mnyama pori aina ya swala ambapo pia imeelezwa kuwa watuhumiwa ni wawindaji haramu katika hifadhi za Taifa mbalimbali hapa nchini.

 

Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili Innocent Mendrad Komba [48] Fundi Selemala, mkazi wa Itunge Kyela na Zawadi Jackson Mwakijolo [32] Mwandishi wa Habari, mkazi wa Mtaa wa Butiama Wilayani Kyela kwa tuhuma za kupatikana na vifurushi 142 vya dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Kilogramu 142.

 

Kamanda Benjamin Kuzaga, amesema watuhumiwa walikuwa wakisafirisha dawa hizo za kulevya kutokea Boda ya Kasumulu wilayani Kyela kuelekea Kyela Mjini kwa kutumia Gari lenye namba za usajili T.969 BLZ aina ya Toyota Vista.

 

Amesema dawa hizo za kulevya zilikuwa kwenye mifuko mitano ya Sandarusi iliyokuwa na nguo mbalimbali za Mtumba na watuhumiwa imedaiwa kuwa ni wasafirishaji na wauzaji wa dawa hizo za kulevya na kuwa watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.

 

Aidha, watuhumiwa wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ambao ni Rawlence Mgala [24], Stephano Mwamlima [22], Nai Mwatendela [23] na Samweli Mwashambwa [24] wote wachimbaji wadogo, wakazi wa Sinjilili wilayani Chunya kwa tuhuma za kuuza madini yadhaniwayo kuwa ni bandia yenye uzito wa gramu 1.41 kwa mnunuzi mdogo aitwaye Jordan Soda, mkazi wa Chunya.

 

Taarifa ya Polisi inasema watuhumiwa wamewahi kufanya tukio kama hilo tarehe 31.12.2024 ambapo waliuza madini bandia gramu 10 na kulipwa kiasi cha shilingi 1,480,000/=. Pia, katika muendelezo wa Misako, alikamatwa mtuhumiwa Cornel Nkeke Mwakibinga [22] mkazi wa Uzunguni Chunya kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya uvunjaji na wizi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.

 

Polisi inatoa rai kwa wananchi kuishi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka kuingia kwenye mkono wa sheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!