Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Juma, ametangaza mabadiliko ya utaratibu wa uendeshaji wa mikutano ya tume hiyo ili kulinda usalama na faragha za waathirika wanaotoa ushahidi.
Akizungumza, Januari 24, 2026, katika ukumbi wa Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Profesa Juma amesema kuwa kuanzia sasa, waandishi wa habari hawataruhusiwa kuwepo wakati waathirika wanapowasilisha ushuhuda wao mbele ya tume hiyo. Hatua hii inakuja baada ya kuibuka kwa malalamiko kuwa taarifa binafsi za waathirika zinasambazwa mitandaoni bila ridhaa yao.
“Kufuatia hali hiyo, utaratibu utakaoendelea kutumiwa ni Tume kueleza kazi zake kwa waandishi wa habari na maudhui kwa ujumla lakini wakati wa kusikiliza waathirika waandishi hawatoruhusiwa ‘mtatupisha”, ameeleza Profesa.
Profesa Juma amebainisha kuwa kusambaa kwa taarifa hizo kumesababisha baadhi ya waathirika kusumbuliwa na maombi ya mahojiano kutoka kwa vyombo mbalimbali vya habari, jambo linalowaletea msongo wa mawazo na changamoto ndani ya familia zao.
“Baadhi ya waathirika wanapigiwa simu wanaombwa kufanya mahojiano ‘interview’ na baadhi ya media jambo ambalo linawaletea msongo wa mawazo, ulinzi wa taarifa za binafsi na usiri na wengine imesababisha changamoto kwa familia zao”, amesisitiza Profesa Juma.
Tume hiyo imeshakamilisha kusikiliza waathirika katika wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, na Ubungo mkoani Dar es Salaam. Baada ya hapa, inatarajiwa kuendelea na mikutano yake katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Ruvuma, na Iringa ili kukusanya taarifa za matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.