Waasi wa kundi la M23 wameimarisha udhibiti wao katika eneo la machimbo ya madini ya coltan, Rubaya, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na wanakusanya kodi ya uzalishaji inayofikia takriban dola 300,000 (Zaidi ya Shilingi za Kitanzania milioni 800) kwa mwezi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezwa Jumatatu. Madini ya coltan yanayochimbwa eneo hilo yanahusishwa na uzalishaji wa simu janja na kompyuta.
Bintou Keita, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, alisema kuwa biashara ya madini kutoka Rubaya inachangia zaidi ya asilimia 15 ya usambazaji wa kimataifa wa tantalum, madini ambayo ni muhimu sana kwa mataifa ya Magharibi. Keita alionesha wasiwasi wake kuhusu namna mapato haya yanavyowapa nguvu zaidi waasi huku raia wakiendelea kuteseka.
Mgogoro wa rasilimali katika eneo la mashariki mwa Kongo umechochea vurugu nyingi tangu kuzuka upya kwa uasi wa M23 mnamo Machi 2022, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na zaidi ya milioni moja kulazimika kuhama makazi yao. Waasi sasa wamekuwa wajasiriamali wa kijeshi, wakinufaika kifedha kupitia udhibiti wa madini.
Keita alihimiza hatua za kimataifa kuchukuliwa dhidi ya wale wanaofaidika na biashara haramu ya madini, akisema kuwa bila vikwazo, amani haitapatikana, na raia wataendelea kuathirika.