Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina amewataka wachimbaji wadogo nchini kuacha kuilalamikia Serikali badala yake waishauri kuhusu wanachokitaka kwa maslahi ya taifa.
Amesema hayo wakati akifungua kongamano la siku ya pili ya Maadhimisho ya Wiki ya Madini mwaka 2024 kwa wachimbaji wadogo ililofanyika katika ukumbi mdogo wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesema kupitia makongamano ya wiki ya Madini mwaka 2024 wayatumie kuishauri serikali mambo mbalimbali kama changamoto za wachimbaji madini wadogo ili serikali itafutie majibu.
“Ndio maana sisi kama Shirikisho tunaandaa makongamano na mikutano maana yake ni kuishauri Serikali na viongozi kwa sababu sisi ndio wenye sekta kwani huwezi kuwa mwanachama wa FEMATA kama siyo mchimbaji wa madini ili uwe na uchungu na kile unachozungumzia” Amesema Bina.
Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki ya NMB Alex Mgeni amewataka wachimbaji wadogo wa madini kujikita katika kuchimba madini mkakati ambayo soko lake ni kubwa ni upande wa kitaifa na kimataifa.
Amesema madini hayo ya kimkakati hutumika sana katika shughuli za kiteknolojia kama utengenezaji betri za magari, maji ya betri na vifaa vya simu hivyo wawekeze kwenye madini hayo waweze kunufaika zaidi.
“Pia wasije kubaki nyuma katika uchimbaji huo wa madini ya kimkakati na wakawaachia wachimbaji wageni kutoka nje wakanufaika maana yake hata mapato mengi hayatabaki Tanzania yataenda nje ya nchi” Amesema Alex.
Mwenyekiti wa Wauzaji na Wanunuzi wa Madini Tanzania (TAMIDA) Othuman Tharia amesema wanakamilisha viwanda viwili vya kuongezea thamani ya madini yenye thamani ili kuwa na uhakika wa soko la madini wanayochimba nchini. Viwanda hivyo vinajengwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga na katika kisiwa cha Zanzibar.
Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo mkoa wa Ruvuma Kasimu Pazi amemtaka Waziri wa Madini, Antony Mavunde atekeleze agizo la Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango la kutomnyang’anya mchimbaji mdogo eneo kumpisha mchimbaji mkubwa kwa kisingizio cha eneo hilo lilikuwa la wachimbaji wakubwa.