Latest Posts

WACHIMBAJI WAHAMASISHWA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

Katika uhakikisha kila mwananchi anatimiza haki yake ya msingi ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi anaemuhitaji, wachimbaji wadogo wa madini Mkoa wa Geita wamehamasishwa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa ifikapo Novemba 27, 2024.
Ameyasema hayo Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA) Bw. Titus Kabuo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuingia ndani ya mgodi wenye urefu wa takribani mita 400 chini ya ardhi katika kuhamasisha wafanyakazi kupata nafasi ya kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ikiwa ni haki yao kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hatua hiyo inalenga kuwapa wafanyakazi nafasi ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia ya nchi, jambo ambalo litapelekea kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Sisi sote tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa sauti zetu zinasikika katika masuala muhimu ya kitaifa na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, hakikisheni mnawahi katika vituo vya kujiandikishia.” amesema Kabuo
Ameongezea kuwa kura ni zana muhimu kwa raia kuleta mabadiliko na kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa anachangia katika mustakabali wa taifa.
Kabuo amesema kuwa kujiandikisha kupiga kura si tu haki bali ni wajibu wa kila mfanyakazi na raia wa Tanzania, kwa kufanya hivyo, anatarajia kuwa wafanyakazi wake watachangia katika kuleta mabadiliko yanayohitajika sio tu katika sekta ya madini bali katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Sote tunatamani kuona nchi yetu ikipiga hatua kubwa za maendeleo, lakini maendeleo hayo hayaji bila sisi kushiriki katika maamuzi muhimu ya kitaifa,” amesema Kabuo.
Aidha, mwenyekiti huyo amewahimiza wafanyakazi wake kuona ushiriki wao katika uchaguzi kama fursa ya kuboresha hali zao za maisha, kwani viongozi wanaochaguliwa wana uwezo wa kubuni sera zitakazoleta mabadiliko katika sekta ya madini na maeneo mengine ya uchumi.
Kauli hiyo ya Kibuo imepokelewa kwa shangwe na wafanyakazi ambao wamesifu jitihada zake za kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi.
Wengi wao wamesema kwamba hawakujua umuhimu wa kujiandikisha kupiga kura, lakini kutokana na mwongozo wa Kibuo, sasa wanaelewa vizuri zaidi umuhimu wa haki yao ya kidemokrasia.
Naye Meneja wa Mgodi wa KABUO GOLD MINE Amos Mwita na baadhi ya wafanyakazi wa Mgodi huo wamesema kuwa wamepokea na wapo tayari kwenda kujiandikisha ili kutimiza haki hao ya msingi na yakidemokrasia lakini zaidi ni kupata nafasi ya kuchagua viongozi ambao wataleta mabadiliko chanya katika sekta ya Madini na Jamii kwa ujumla wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!