Na Theophilida Felician.
Wadau wa maji kata Kanyigo halmashauri ya Missenyi mkoani Kagera wamejikuta wakivunja kikao ghafla cha bodi ya maji kilichokuwa kimeandaliwa na bodi hiyo na kufanyika shule ya sekondari ya kiislamu Kanyigo hii tarehe 11 Julai, 2024 kutokana na mtendaji wa kata Daudi Kyaka kutoa tamko la amri ya kuwaondao kwenye kikao waandishi wa habari wawili waliokuwa wamealikwa na bodi hiyo ya maji kutoka Redio Karagwe na Kasibante kushiriki kikao hicho.
Hali hiyo imetokea muda mfupi kuanza kwa kikao afisa huyo amesimama na kuanza kutoa amri hiyo akidai kwamba maagizo hayo amepewa na mkuu wa wilaya. Tamko hilo wananchi hawakuwa tayari kukubaliana nalo huku wakimuhoji kwanini anawafukuza wandishi wa habari.
“Jambo la Mkuu wa Wilaya sitaki kuweka mjadala hivyo waondoke! waondoke! hatuwahitaji” Mtendaji Daudi amesisitiza mbele ya wadau hao.
Kutokana na sintofahamu hiyo iliyojitokeza muda mfupi kuanza kwa kikao na kuwasili kwa watumishi wa Wakala ya Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Missenyi, wadau hawakukawia wakachukua maamuzi ya kutoka ndani ya ukumbi na kutawanyika wakiashiria kutokukubali kitendo kilichotekelezwa na mtendaji.
Baadhi ya wadau baada ya kutawanyika wameelezea kusikitishwa na kitendo hicho ambapo wameomba serikali kushughulikia suala hilo kwani halina nia njema katika ujenzi wa maendeleo ya wananchi.
Wameongeza kwamba mradi wa Kanyigo umekuwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea wananchi kutokupata maji kwa ufasaha.
Wamehitimisha wakifafanua kuwa kwenye kikao hiko zaidi ilikuwa ni kutaka kujadili changamoto zinazoukabili mradi wa maji Kanyigo hivyo wameshangazwa ni kitu gani kinachofichwa kwa vyombo vya habari.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga akizungumza kwa njia ya simu amekanusha kuhusika na agizo hilo.