Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 5 Juni, wadau wa mazingira katika Kata ya Wazo, na maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam, wamejitokeza kushiriki maadhimisho hayo kwa kupanda miti katika maeneo ya taasisi za elimu na afya.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Elimu wa Kata ya Wazo, Novatus Rwemera, alisema kuwa suala la utunzaji wa mazingira halijaanza leo, bali limekuwa likipewa kipaumbele tangu kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari Mivumoni.
“Kuanzishwa kwa shule ya Mivumoni, suala kubwa limekuwa ni kulea wanafunzi kwa kuwapa elimu ya utunzaji wa mazingira, si tu ndani ya shule bali hata katika maeneo wanakotokea,” amesema Rwemera.
Aidha, Rwemera alitoa wito kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kuendeleza juhudi za kutunza mazingira yao kwa kupanda miti, akisisitiza umuhimu wa kupanda miti ya matunda badala ya miti ya kivuli pekee kwa sababu ya faida zake za kiafya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzania Social Initiative for Development Organisation (TSID), George Tibesigwa, alisema kwamba taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza mikakati ya kupanda miti kama sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali ya elimu na afya.
“Tumeweza kupanda miti katika shule ya sekondari Mivumoni, shule ya msingi Pwani, shule ya msingi Mkoani, Kisauke Sekondari, Dany Chongolo na Zahanati ya Salasala. Lengo letu ni kuhakikisha jamii inaelimishwa na kushirikishwa katika kutunza mazingira,” amesema Tibesigwa.
Naye Happyness Mshana, ambaye ni mdau wa mazingira, alisisitiza kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira yasitazamwe kama tukio la siku moja, bali yawe kichocheo cha mabadiliko chanya katika jamii.
“Jukumu la kutunza mazingira si la serikali pekee au walimu, bali kila mmoja wetu anawajibika. Miti inapopandwa leo, matokeo yake yataonekana miaka ijayo,” amesema Mshana.
Zoezi la upandaji miti limefanyika kwa ushirikiano wa wanajumuiya ya shule, viongozi wa kata, wanafunzi na wazazi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.