Wadau wa utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameiomba serikali kuchukua hatua za kudumu katika ujenzi wa barabara ndani ya hifadhi hiyo, hususan barabara ya Serengeti, ili kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo na kupunguza changamoto zinazotokana na idadi kubwa ya magari yanayopita kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha, alisifu hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) katika kuboresha barabara hizo. Alieleza kuwa kwa wastani, magari 600 hupita kwenye barabara hizo kila siku, hali inayochangia kuharibika kwa miundombinu hiyo.
Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.

“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi, mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili magari ni mengi sana na ndiyo chanzo kikuu cha ukorofi wa barabara hii”, ameeleza Macha.
Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika ili kupunguza adha hiyo kwa wageni.

“Shirika limeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.
Pia, Kamishna Kuji alibainisha kuwa TANAPA inafanya jitihada za haraka kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi zote za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia tekinolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na idadi ya magari yanayotumia barabara hiyo.
“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote, tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu, hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephen Msumi alisema kuwa menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika hifadhi ikiwemo kudhibiti mwendokasi pamoja na kuzingatia alama mbalimbali za barabara ili kuepusha madhara yanayojitokeza kwa kutozingatia sheria hizo.
Hifadhi ya Taifa Serengeti inafanya ukarabati wa barabara zake ili kuondoa adha hiyo na kuzifanya barabara zote ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.