Latest Posts

WAFANYABIASHARA SOKO KA MJIMPYA MORO WAOMBA KUBORESHEWA MIUNDOMBINU

Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Mji Mpya, mkoani Morogoro, wakiongozwa na Mwenyekiti wa soko hilo, Abdalla Mfaume, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya soko hilo kutokana na uchakavu mkubwa uliopo, hali inayowaathiri katika shughuli zao za kila siku za biashara.

Wafanyabiashara hao walitoa ombi hilo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Kata hiyo iliyofanyika kwa lengo la kukagua na kufuatilia maendeleo ya miradi mbalimbali. Wamesema kuwa soko hilo lilijengwa tangu kipindi cha ukoloni, na tangu hapo halijafanyiwa maboresho makubwa, jambo linalosababisha miundombinu yake kuwa chakavu na isiyokidhi mahitaji ya sasa.

Aidha, wameeleza kuwa uboreshaji wa soko hilo utasaidia kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza usalama wa bidhaa zao pamoja na kuwapa uhuru zaidi wa kufanya shughuli zao bila vikwazo vinavyotokana na hali mbaya ya miundombinu.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa soko hilo, Abdalla Mfaume, amebainisha kuwa pamoja na uchakavu wa majengo, soko hilo pia linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji katika vyoo. Amesema hali hiyo si salama kiafya kwa wafanyabiashara na wateja, na inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ya mlipuko endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kata hiyo, Kombo Hussen Nkumilwa, amesema kuwa soko hilo ni la muda mrefu na limepitwa na wakati. Akieleza kuwa wakati wa msimu wa mvua, soko hilo hukumbwa na changamoto kubwa ya maji kujaa katika maeneo ya biashara, hadi kufikia meza za wafanyabiashara, hali inayosababisha hasara na usumbufu mkubwa.

Kutokana na hali hiyo, Nkumilwa ameiomba Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kulipa kipaumbele suala la uboreshaji wa soko hilo ili kuwaondolea wananchi adha wanazokutana nazo.

Naye Diwani wa kata hiyo, Iddi Mussa, amesema kuwa amepokea maombi ya wafanyabiashara na wananchi kwa uzito unaostahili, na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi. Alieleza kuwa kuna mipango ya kujenga soko la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara, likiwa na miundombinu bora ikiwemo mifumo ya maji, mifereji ya maji ya mvua, pamoja na vyoo vya kisasa.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!